
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, kwa niaba ya Wizara ya Afya, ametangaza nafasi 63 za ajira za mkataba wa mwaka mmoja kwa Watanzania wenye sifa na uwezo wa kujaza nafasi hizo.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa Julai 9, 2026, nafasi hizo zinahusisha Madaktari Daraja la II (Medical Officer II) 23 na Maafisa Wauguzi Daraja la II (Assistant Nursing Officer II) 40.
Kwa upande wa Madaktari Daraja la II, waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Udaktari kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali pamoja na kuwa wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika (Medical Council of Tanganyika). Watakaoajiriwa watakuwa na jukumu la kutoa huduma za matibabu, kushiriki katika utafiti, kuzuia na kudhibiti milipuko ya magonjwa, kusimamia watumishi walio chini yao pamoja na kuboresha huduma za afya katika maeneo yao ya kazi.
NAFASI ZA KAZI ZA MKATABA WIZARA YA AFYA 09-07-2026
Kwa Maafisa Wauguzi Daraja la II, waombaji wanapaswa kuwa na Stashahada (Diploma) ya Uuguzi kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali na kusajiliwa na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania. Majukumu yao ni pamoja na kutoa huduma za uuguzi, kukusanya takwimu za afya, kutoa elimu kwa wagonjwa na jamii, pamoja na huduma za kinga na uzazi.
Sekretarieti ya Ajira imeeleza kuwa waombaji wote wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wenye umri usiozidi miaka 45, isipokuwa kwa nafasi zinazohusu taasisi za kijeshi ambapo masharti maalumu ya umri yanazingatiwa. Pia waombaji wanatakiwa kuambatisha nyaraka zote muhimu, ikiwemo vyeti vya taaluma, cheti cha kuzaliwa kilichothibitishwa na Mwanasheria au Wakili, pamoja na barua ya maombi iliyosainiwa.
Maombi yote yanapaswa kutumwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa Ajira (Recruitment Portal), huku mwisho wa kutuma maombi ukiwa Julai 18, 2026.
Sekretarieti ya Ajira imekumbusha kuwa mchakato wa ajira unazingatia misingi ya haki, usawa na uwazi, na imeonya kuwa ni marufuku kutoa au kupokea rushwa kwa lengo la kupata ajira au kupangiwa kituo cha kazi. Aidha, waombaji watakaowasilisha taarifa au nyaraka za kughushi watachukuliwa hatua za kisheria.
NAFASI ZA KAZI ZA MKATABA WIZARA YA AFYA 09-07-2026