
Wakati wengi huingia kwenye ndoa wakiamini ni mwanzo wa maisha mapya yaliyojaa upendo, kwa baadhi ya wanaume nchini Iran safari hiyo ilidaiwa kugeuka mwisho wa maisha yao. Kwa zaidi ya miaka 20, mfululizo wa vifo vya wanaume mbalimbali haukuibua mashaka makubwa, hadi kifo cha mwisho kilipoibua uchunguzi uliofichua moja ya kesi zilizotikisa taifa hilo. Katikati ya kesi hiyo alikuwapo mwanamke aitwaye Kulthum Akbari, ambaye baadaye alikabiliwa na mashtaka mazito ya mauaji ya waume 11.
Kwa mujibu wa mamlaka za Iran, uchunguzi ulioanzishwa baada ya kifo cha mume wake wa mwisho mwaka 2023 ulifichua mazingira yaliyowafanya wachunguzi kurejea vifo vya waume wengine aliowahi kuwa nao. Uchunguzi huo ulipelekea madai kwamba kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20, wanaume kadhaa waliomuoa walifariki katika mazingira yaliyofanana.
Waendesha mashtaka walidai kuwa Kulthum aliwalenga zaidi wanaume wazee waliokuwa na mali au waliokuwa wakiishi peke yao. Baada ya kujenga uhusiano wa karibu na kufunga ndoa, ilidaiwa kuwa baadhi yao walifariki muda mfupi baadaye, jambo lililozua mashaka makubwa baada ya historia ya ndoa zake kuchunguzwa kwa kina.

Kesi hiyo ilivuta hisia za wananchi wengi nchini Iran, huku wachunguzi wakisema ushahidi uliokusanywa ulihusisha vifo vya waume 11. Uchunguzi uliendelea kwa muda mrefu ukihusisha ushahidi wa kitabibu, vielelezo na mahojiano na mashahidi mbalimbali.
Mwaka 2025, mahakama nchini Iran ilimkuta na hatia kwa makosa 11 ya mauaji. Alipokea hukumu 10 za adhabu ya kifo, huku katika kesi moja familia ya mwathirika ikikubali fidia badala ya adhabu hiyo. Pia alihukumiwa kifungo cha miaka 10 kwa kosa la jaribio la mauaji.
Kesi ya Kulthum Akbari imeendelea kutajwa kama mojawapo ya kesi zilizotikisa Iran katika miaka ya hivi karibuni, ikizua maswali kuhusu namna mauaji hayo yalivyoweza kudumu kwa muda mrefu bila kugunduliwa na mamlaka.