×

Airtel Yaimarisha Upatikanaji Wa Huduma Za Kidijitali Kwa Wananchi Kwa Ajili Ya Kukuza Uchumi Endelevu


Dar es Salaam, 15 Julai, 2026 – Airtel Tanzania imezindua duka la kisasa la Airtel eneo la Shekilango lililopo Wilaya ya Ubungo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kifedha kwa njia ya kidigitali inayofahamika kama Airtel Kila Kona.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Airtel Tanzania Bi. Adriana Lyamba alisema Airtel inaendelea kuwekeza katika maduka ya kisasa, teknolojia na mifumo ya kidigitalu ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora, za haraka na zinazokidhi mahitaji ya wateja.

“Sisi, Airtel Tanzania, tunaamini kuwa huduma bora inaanza kwa kusikiliza mahitaji ya wateja na kuwafikia walipo. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika maduka ya kisasa, mifumo ya kidijitali, teknolojia na watu wetu ili kuhakikisha kila mteja anapata huduma ya haraka, sahihi na kwa ukaribu zaidi,” alisema.

Alitaja kuwa Shekilango ni moja ya maeneo yanayokuwa kwa kasi na ni kitovu cha biashara, usafirishaji na makazi, kutokana na shughuli hizi mahitaji ya huduma za mawasiliano, huduma za kifedha kwa njia za kidigitali ni muhimu.

Kupitia duka hili, wananchi wa Shekilano na maeneo ya jirani watapata huduma zote za Airtel katika sehemu moja, ikiwemo usajili wa laini, huduma za Airtel Money, Intaneti, Simu janja, pamoja na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa watoa huduma kwa wateja wanaopatikana papo hapo.

Kwa upande wake, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando, aliipongeza Airtel Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kupanua huduma za kidijitali, hatua zinazochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali na maendeleo endelevu nchini.

“Tunajivunia kile Airtel Tanzania imekifanya kwa kuchangia gawio la Shilingi Bilioni. 65.48 kwa Serikali na bado inaendelea kuchangia maendeleo ya taifa kwa kufanya uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano na huduma za kidigitali kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu,” alisema Mhe. Msando.

Katika kuendeleza uwajibikaji kwa jamii na mazingira, Airtel Tanzania pia inaendelea kutekeleza kampeni ya Go Green, inayolenga matumizi ya nishati safi na usimamizi endelevu wa mazingira. Kupitia mradi wa E-Waste Go Green, Airtel inaendelea kuhamasisha ukusanyaji na urejelezaji salama wa taka za vifaa vya kielektroniki ili kulinda afya za wananchi na mazingira.

Sambamba na hilo, kwa sasa zaidi ya asilimia 50 ya minara ya mawasiliano ya Airtel nchini imeunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa. Hatua hii imechangia kupunguza matumizi ya mafuta, kuongeza matumizi ya nishati safi, na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, hatua ambayo inaunga mkono jitihada za kulinda mazingira.

Airtel Tanzania ilisisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali na kuboresha huduma kwa wateja, ili kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa njia za kidijitali, kuchochea shughuli za kiuchumi, na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.

Airtel Tanzania inamilikiwa kwa asilimia 49 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivi karibuni, kampuni ilikabidhi gawio la shilingi bilioni 65.48 kwa Serikali, hatua inayoakisi mchango wake katika kukuza uchumi endelevu wa taifa kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano na huduma za kidijitali.

Leave a Comment