×

Video: Maopena Akamatwa kwa Tuhuma za Kumuua Baba Yake na Baba Mdogo

Dar es Salaam – Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Osam Hamza, maarufu kwa jina la Maopena, kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi pamoja na baba yake mdogo katika tukio lililotokea eneo la Sindano, Mwananyamala Kisiwani, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Julai 18, 2026, mtuhumiwa alikamatwa Julai 17, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri katika eneo la Makongo baada ya kukutwa akiwa na kisu kilichokuwa na damu pamoja na mavazi yaliyokuwa yamechafuliwa damu.

Baada ya kukamatwa, alipelekwa katika kituo cha Polisi kwa ajili ya mahojiano na uchunguzi zaidi.

Polisi wamesema wakati mahojiano na mtuhumiwa yakiendelea, majira ya saa 4:00 usiku walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kupitia Kituo cha Polisi Oysterbay kuwa watu watatu waliokuwa wanaishi katika nyumba moja eneo la Sindano, Mwananyamala, walikuwa hawaonekani huku kukiwa na damu nyingi ndani ya nyumba hiyo.

Kutokana na taarifa hiyo, timu za uchunguzi pamoja na wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi zilifika eneo la tukio na kuanza kufanya uchunguzi.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa watu wawili, Hamza Juma Omari maarufu Mautila (48) na Ally Juma Omari (37), ambao walikuwa miongoni mwa watu watatu waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo, walikuwa wameuawa na miili yao kufukiwa ndani ya shimo katika eneo la makazi yao.

Kwa mujibu wa Polisi, mtuhumiwa Osam Hamza, ambaye ni mtoto wa marehemu Hamza Juma Omari, ndiye anayehusishwa na mauaji hayo. Hata hivyo, chanzo au sababu iliyosababisha tukio hilo bado haijafahamika na inaendelea kuchunguzwa.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira yote ya tukio hilo kabla ya hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

Aidha, Polisi wamewashukuru wananchi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano wao katika kutoa taarifa zilizowezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa na kufanikisha uchunguzi wa tukio hilo.

Tukio hilo limezua mshtuko mkubwa kwa wakazi wa Mwananyamala Kisiwani na maeneo ya jirani, huku wengi wakisubiri matokeo ya uchunguzi yatakayobainisha kilichopelekea mauaji hayo ya watu wa familia moja.

Leave a Comment