
Tovuti rasmi ya Rais wa Kenya, William Ruto, imedukuliwa huku wadukuzi wakiondoa maudhui ya kawaida ya ukurasa wa mwanzo na kuweka ujumbe wa vitisho unaomtaka Rais kulipa fidia kwa njia ya sarafu ya kidijitali ya Bitcoin.
Ukaguzi wa tovuti hiyo (president.go.ke) ulionyesha kuwa ukurasa huo ulikuwa umebadilishwa na kuwekwa ujumbe unaodai kuwa ni onyo kwa Rais Ruto, ukiambatana na anwani ya mkoba wa cryptocurrency na maelekezo ya kufanya malipo.
Katika ujumbe huo, wadukuzi walidai Bitcoin 5 huku wakitishia kutoa taarifa walizodai kuwa wanazo kuhusu Rais iwapo malipo hayo hayatafanyika ndani ya muda walioutoa.
“Huu ni ujumbe wa tatu kwako; kabla hatujavujisha kila kitu kukuhusu. Fanya malipo ya Bitcoin 5 kwenye mkoba wa Bitcoin…” ulisomeka ujumbe huo.
Ikulu ya Kenya imethibitisha kufahamu kuhusu tukio hilo na kusema timu yake ya teknolojia ya habari (TEHAMA) ilikuwa tayari ikishughulikia tatizo hilo.
Kwa thamani ya sasa ya Bitcoin, madai hayo ya Bitcoin 5 yanaweza kufikia zaidi ya shilingi milioni 41 za Kenya, sawa na zaidi ya shilingi milioni 838 za Tanzania.
Wadukuzi hao pia walibadilisha muonekano wa ukurasa huo kwa kuweka ujumbe wao juu ya picha ya nyuma iliyokuwa na chapa rasmi ya Ikulu, huku wakitaja majina ya watu watatu katika ujumbe huo.
Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu usalama wa mifumo ya kidijitali ya serikali ya Kenya, hasa kutokana na kutokuwa wazi kama udukuzi huo uliathiri ukurasa wa mbele pekee au uliingia kwenye mifumo ya ndani ya tovuti.
Si mara ya kwanza kwa mifumo ya serikali ya Kenya kushambuliwa mtandaoni. Novemba mwaka jana, tovuti kadhaa za wizara na taasisi za serikali zililengwa katika shambulio lililosababisha baadhi ya huduma za mtandaoni kutopatikana na maudhui rasmi kubadilishwa.
Hata hivyo, baadhi ya taasisi muhimu kama Wizara ya Ulinzi na Hazina ya Taifa ziliripotiwa kutokumbwa na athari za shambulio hilo.