
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imeagiza Jeshi la Magereza kumfikisha Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, moja kwa moja ndani ya chumba cha Mahakama kabla ya majaji kuingia wakati wa kuendelea kusikiliza shauri la kikatiba kuhusu haki za mawakili kumtembelea gerezani. Mahakama pia ilieleza kuwa kwa kuwa ni shauri la kikatiba na si la jinai, Lissu ana haki ya kuketi kwenye viti vya mawakili badala ya kizimba, ingawa alisema hana pingamizi kuendelea kukaa humo.
Katika usikilizwaji wa shauri hilo lililofunguliwa na mawakili Kulwa William Maduhu, Nashon Kungu na Paul Kisabo dhidi ya Mamlaka ya Magereza, shahidi wa kwanza Kulwa Maduhu alitoa ushahidi akithibitisha kuwa yeye na mawakili wenzake waliwahi kunyimwa nafasi ya kuzungumza kwa faragha na Lissu gerezani, huku baadhi yao wakizuiwa kuingia licha ya kuwa mawakili wake. Alikiri pia kuwa Mahakama ilitambua mawakili hao kama wasaidizi wa Lissu baada ya kuamua kujitetea mwenyewe.
Katika mahojiano yake, Lissu alidai ushahidi uliotolewa unaonyesha kuwepo kwa ubaguzi dhidi ya mawakili wa kujitegemea, akisema walikuwa wakifanyiwa upekuzi mkali na mazungumzo yao ya faragha na mteja wao kusikilizwa na maafisa wa gereza, jambo alilosema linakiuka haki za msingi za mawasiliano kati ya wakili na mteja. Baada ya kumaliza ushahidi wa shahidi wa kwanza na kuanza maswali ya upande wa walalamikiwa, Mahakama iliahirisha shauri hilo hadi kesho saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa shahidi wa pili.