
Nyuma ya mafanikio makubwa ya baadhi ya mastaa wa Kombe la Dunia 2026 kuna simulizi za mapenzi zilizoanza tangu utotoni. Wakati wengi walikutana baada ya kuwa maarufu, wachezaji hawa waliwapata wenzi wao kabla ya umaarufu, fedha na mafanikio makubwa ya soka.
Hawa ndio mastaa watano waliooa wapenzi wao wa utotoni.
1. Lionel Messi na Antonela Roccuzzo
Nahodha wa Argentina, Lionel Messi, alikutana na mke wake Antonela Roccuzzo wakiwa watoto katika mji wa Rosario nchini Argentina. Wawili hao walitengana kwa muda Messi alipohamia Hispania kuendelea na soka, lakini walikutana tena mwaka 2005.
Baada ya miaka kadhaa ya uhusiano, walifunga ndoa Juni 2017 katika harusi iliyotajwa kuwa miongoni mwa harusi kubwa zaidi katika historia ya Argentina. Leo hii wana watoto watatu wa kiume, Thiago, Mateo na Ciro.

2. Harry Kane na Katie Goodland
Nahodha wa England, Harry Kane, alimfahamu mke wake Katie Goodland tangu walipokuwa watoto.
Wawili hao walisoma pamoja na hata kuhudhuria sherehe ya kuhitimu shule ya sekondari (prom) wakiwa pamoja. Kane aliwahi kumwambia Katie akiwa mdogo kuwa siku moja angekuwa nahodha wa timu ya taifa ya England, jambo ambalo lilitimia mwaka 2018.
Walifunga ndoa mwaka 2019 na sasa wana watoto wanne.

3. Jordan Pickford na Megan Pickford
Kipa wa England Jordan Pickford alianza uhusiano na Megan Pickford walipokuwa vijana.
Walikutana walipokuwa wakisoma katika Shule ya St Robert of Newminster nchini England. Jordan alikuwa na miaka 16 huku Megan akiwa na miaka 14 walipoanza kutoka kimapenzi.
Walifunga ndoa mwaka 2020 na sasa wamebarikiwa watoto watatu.

4. Gio Reyna na Chloe Reyna
Nyota wa Marekani Gio Reyna na mke wake Chloe Reyna walikulia pamoja nchini Marekani huku wote wakicheza soka tangu wakiwa watoto.
Wawili hao walifunga ndoa Julai 2025 na kwa sasa wanatarajia kupata mtoto wao wa kwanza. Katika Kombe la Dunia 2026, Gio aliweka wazi habari hizo baada ya kushangilia bao lake kwa kuweka mpira tumboni na kunyonya kidole gumba, ishara ya ujauzito wa mke wake.

5. Ronwen Williams na Roshni
Nahodha na kipa wa Afrika Kusini Ronwen Williams amekuwa akimfahamu mke wake Roshni tangu wakiwa wadogo.
Wawili hao walikulia katika mtaa mmoja mjini Gqeberha na walikuwa marafiki wakubwa kabla ya kuanza uhusiano wa kimapenzi.
Roshni amesema walikuwa wakicheza pamoja soka na kriketi mitaani kabla ya mapenzi yao kukua. Kwa sasa wameoana na wana watoto wawili.
Mapenzi ya mastaa hawa yanaonyesha kuwa mafanikio makubwa ya soka hayajabadilisha uhusiano wao, kwani waliamua kuendelea na watu waliowajua tangu utotoni na kujenga familia imara pamoja.