
Msanii wa Singeli, Meja Kunta, ameomba msaada wa kifedha baada ya kuweka wazi kuwa baba yake amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), akipigania maisha.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Meja Kunta amesema hali ya baba yake ni mbaya na amefikia hatua ya kuamua kuuza mali zake ili kugharamia matibabu.
Msanii huyo amesema yuko tayari kuuza viwanja, nyumba, magari pamoja na mali nyingine alizonazo, akisisitiza kuwa kwake mali si muhimu kuliko uhai wa baba yake.

“Nauza viwanja, nyumba, magari na mali zangu nyingine. Bora mali ziende, lakini baba yangu apate nafasi ya kuendelea kuishi,” ameandika.
Meja Kunta ameeleza kuwa tayari alimpoteza mama yake miaka iliyopita, hivyo baba yake ndiye mzazi pekee aliyebaki, jambo linalomfanya afanye kila linalowezekana kuhakikisha anapata matibabu.
Baada ya ujumbe huo kusambaa mitandaoni, mashabiki na wadau mbalimbali wameendelea kumfariji na kumtakia baba yake nafuu, huku wengine wakijitokeza kuonesha utayari wa kumsaidia katika kipindi hiki kigumu.
Meja pia amewahimiza watu wanaoweza kununua mali anazouza au kumsaidia kwa njia nyingine yoyote kuwasiliana naye moja kwa moja kupitia ujumbe binafsi (DM) au simu ili kusaidia kuokoa maisha ya baba yake.
