×

Kijana Ahukumiwa Kifungo cha Miaka 25 kwa Kumuua Binti wa Miaka 17 kwa Risasi

Kijana Michael Garcia.

Kijana Michael Garcia amehukumiwa kifungo cha miaka 25 baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi wa shule ya sekondari mwenye umri wa miaka 17, Danyelisse Pabon-Cubero, kwa risasi iliyompata kimakosa wakati akimlenga mtu mwingine.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, tukio hilo lilitokea Aprili 30, 2025, nje ya nyumba moja katika eneo la Alphonse Street, Rochester, New York, ambapo Garcia, aliyekuwa na umri wa miaka 18 wakati huo, alifyatua risasi kadhaa kufuatia ugomvi uliodaiwa kuhusishwa na maziwa ya watoto wachanga (baby formula).

Lengo la shambulio hilo lilikuwa mwanaume mwingine mwenye umri wa miaka 36, lakini moja ya risasi iliingia ndani ya nyumba na kumpiga Danyelisse kichwani. Msichana huyo hakuwa sehemu ya ugomvi huo na baadaye alifariki kutokana na majeraha aliyopata.

Mwanafunzi wa shule ya sekondari mwenye umri wa miaka 17, Danyelisse Pabon-Cubero enzi za uhai wake.

Baada ya tukio, Garcia alikimbia lakini alikamatwa muda mfupi baadaye na polisi katika eneo la Brockport, takribani kilomita 32 kutoka Rochester.

Waendesha mashtaka walisema kitendo cha Garcia cha kufyatua risasi kuelekea kwenye nyumba kiliharibu maisha ya familia nyingi na kumwacha mwathirika mwingine akiwa na majeraha makubwa ya kudumu.

Familia ya Danyelisse ilimkumbuka kama msichana mwenye ndoto kubwa, aliyetamani kuwa zimamoto, huku pia akiwa mshiriki wa michezo mbalimbali na vikundi vya ngoma shuleni.

Kocha wake wa ngoma, Dasia Johnson, alisema ameridhishwa kuona haki imetendeka, ingawa hakuna hukumu inayoweza kufuta maumivu ya kuondokewa na msichana huyo.

Leave a Comment