×

Mashabiki Milioni 1.8 Wamiminika Madrid Kumpongeza Hispania Baada ya Kutwaa Kombe la Dunia

Madrid, Hispania – Jiji la Madrid liligeuka kuwa bahari ya furaha baada ya takribani mashabiki milioni 1.8 kujitokeza kusherehekea ushindi wa timu ya taifa ya Hispania iliyotwaa Kombe la Dunia 2026.

Hispania iliibuka mabingwa wa dunia baada ya kuifunga Argentina bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Jumapili, Julai 19, kwenye New York New Jersey Stadium, Marekani.

Siku iliyofuata, Jumatatu Julai 20, wachezaji wa Hispania walifanya gwaride kubwa la ushindi kupitia mitaa ya Madrid wakiwa kwenye basi maalum la wazi (open-top bus), huku maelfu ya mashabiki wakijitokeza kuwakaribisha mashujaa wao.

Nahodha wa Hispania, Rodri, alionekana akiwa amebeba kombe la dunia juu huku akishangiliwa na umati mkubwa uliokusanyika katika eneo la Plaza de Cibeles.

Kabla ya kuanza gwaride hilo, kikosi cha Hispania kilikutana na Mfalme Felipe VI, Malkia Letizia pamoja na mabinti wao Princess Leonor na Princess Sofía katika Ikulu ya Zarzuela, kisha wakatembelea Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez, katika makazi rasmi ya serikali.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Rodri alisema kushinda kwa ajili ya nchi yake ni jambo kubwa zaidi katika soka.

“Kushinda kwa ajili ya nchi yako ni kitu kizuri zaidi kilichopo,” alisema Rodri.

Alisema kizazi chao kilikua kikitazama mastaa kama Iker Casillas na Andrés Iniesta wakinyanyua Kombe la Dunia mwaka 2010, na sasa wao wamefanikiwa kufanya jambo hilo hilo.

Mfalme Felipe VI aliuelezea ushindi huo kama “ushindi wa kihistoria”, akiwapongeza wachezaji kwa kuvumilia changamoto na hatimaye kulirudisha kombe hilo nchini Hispania.

Katika fainali hiyo, Hispania ilipata bao la ushindi kupitia Ferran Torres dakika ya 106, na kuandika historia nyingine kubwa kwenye soka la dunia.

Hata hivyo, baada ya filimbi ya mwisho, mchezo huo ulihitimishwa na vurugu za wachezaji uwanjani, huku FIFA ikitarajiwa kuchunguza matukio hayo na kuchukua hatua za kinidhamu endapo itabainika kulikuwa na makosa.

Leave a Comment