×

Waziri Masauni Ahimiza Wananchi wa Rufiji Kutumia Fursa ya Biashara ya Hewa ya Ukaa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, amewahimiza wananchi na viongozi wa Wilaya ya Rufiji kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na biashara ya hewa ya ukaa ili kulinda mazingira na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.

Akizungumza Rufiji Julai 21, 2026, Masauni alisema uhifadhi wa misitu iliyopo wilayani humo ni rasilimali muhimu inayoweza kuwanufaisha wananchi kupitia mpango wa biashara ya hewa ya ukaa unaotekelezwa kimataifa.

Ameeleza kuwa mpango huo unatoa manufaa ya kifedha kwa jamii huku ukiimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Waziri huyo pia ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kushirikiana na wataalamu kuandaa miradi endelevu itakayowawezesha wananchi kunufaika zaidi na fursa zilizopo katika sekta ya mazingira. Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayohakikisha wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na rasilimali zao.

Katika hatua nyingine, Masauni amewapongeza wananchi pamoja na viongozi wa wilaya hiyo kwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudumisha amani na utulivu, hali ambayo imechangia kukuza shughuli za kiuchumi.

Akikumbushia machafuko yaliyowahi kutokea miaka iliyopita, aliwataka wananchi kuendeleza mshikamano na ushirikiano ili kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema sekta ya elimu mkoani humo imeendelea kufanya vizuri, akieleza kuwa shule nne za Mkoa wa Pwani zimefanikiwa kuingia katika orodha ya shule kumi bora kitaifa katika matokeo ya Kidato cha Sita.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba, ameeleza kuwa wilaya hiyo imepata mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani baada ya kufikia Shilingi bilioni 11.6, sawa na kuvuka lengo la Shilingi bilioni 6.7 lililokuwa limewekwa.

 

Leave a Comment