
Washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika kwa msimu wa 10 wanatarajiwa kutangazwa Julai 24, 2026 jijini Dar es Salaam, baada ya waandaaji kutangaza orodha fupi ya miswada saba katika vipengele vitatu vya ushindani.
Tuzo hiyo inayodhaminiwa na Safal Group kupitia kampuni zake tanzu za Mabati Rolling Mills (Kenya) na ALAF Limited (Tanzania), inalenga kutambua na kukuza kazi za fasihi za lugha za Kiafrika pamoja na kuhamasisha tafsiri za lugha hizo.
Kwa mwaka huu, tuzo hiyo inaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, ikiwa imeendelea kutolewa kila mwaka isipokuwa mwaka 2020 kutokana na janga la COVID-19.
Akizungumza wakati wa kutangaza orodha ya washindani waliofika hatua ya mwisho, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi, alisema hatua hiyo ni sehemu ya kusherehekea mafanikio ya safari ya miaka 10 ya tuzo hiyo.

“Tunapotangaza orodha hii fupi, tunayo furaha kuadhimisha miaka 10 ya tuzo hii. Hii ni hatua kubwa iliyopigwa na Safal Group kupitia ALAF Limited Tanzania na Mabati Rolling Mills ya Kenya,” alisema.
Kwa upande wa zawadi, washindi watapata:
- Riwaya mshindi wa kwanza: Dola 5,000 za Marekani
- Riwaya mshindi wa pili: Dola 2,500
- Ushairi mshindi wa kwanza: Dola 5,000
- Ushairi mshindi wa pili: Dola 2,500
- Hadithi fupi: Dola 2,500
Aidha, kazi zitakazoshinda zitapata nafasi ya kuchapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota Publishers.
Orodha ya washiriki waliofika hatua ya mwisho ni pamoja na:
Riwaya
- Ziaka Imetoboka – Mathew Theuri Maina (Kenya)
- Mwanamkasi Ndio Basi – Salim Hussein Ng’anzi (Tanzania)
- Shamba la Mawe – Dickson Damas Mtalaze (Tanzania)
Ushairi
- Diwani ya Vizikwa Vya Kale – Ali Hilal Ali (Tanzania)
- Zigo la Kichwa – Maimuna Hashim Maalim (Tanzania)
- Rima la Miiko na Balaa – Lenard Barnaba Mtesigwa (Tanzania)
Mikusanyiko ya Hadithi Fupi
- Mbunge Mtarajiwa na Hadithi Nyingine – Dominic Maina Oigo (Kenya)
- Koti la Karani na Hadithi Nyingine – Stallone Joyfully (Tanzania)
- Siri ya Mama na Hadithi Nyingine – Sophia Said Puta (Tanzania)
Mwenyekiti wa jopo la majaji, Profesa Rayya Timammy kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema ushindani wa mwaka huu ulikuwa mkubwa kutokana na idadi kubwa ya kazi bora zilizowasilishwa.
Kwa mwaka huu, jumla ya kazi 230 kutoka mataifa saba ziliwasilishwa kuwania Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika. Sherehe za utoaji wa tuzo hizo zitafanyika katika ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.