×

Yanga Yatikisa kwa Kumtambulisha Simo Dladla na Kagisho Dikgacoi

Klabu ya Yanga leo Julai 21, 2026 imeendelea kuimarisha benchi lake la ufundi kwa kuwatambulisha Simo Dladla kuwa kocha msaidizi na Kagisho Dikgacoi kuwa mtaalamu wa mipira iliyokufa (set pieces), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.

Simo Dladla atafanya kazi kwa karibu na kocha mkuu Manqoba Mngqithi, akileta uzoefu alioupata katika vilabu mbalimbali vya Afrika Kusini.

Katika historia yake ya ukocha, Dladla alikuwa kocha msaidizi wa AmaZulu FC msimu wa 2025/26, kabla ya hapo akiwa kocha mkuu wa Maritzburg United, ambayo baadaye ilibadilishwa jina kuwa Durban City FC, kati ya mwaka 2023 na 2025. Pia amewahi kuinoa Uthongathi FC, Richards Bay FC na Real Kings FC, huku mwaka 2019 akihudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi wa Real Kings.

Mafanikio yake makubwa ni kuiongoza Maritzburg United katika harakati za kupanda daraja kuelekea Ligi Kuu ya Afrika Kusini, jambo lililomjengea sifa kama mmoja wa makocha vijana wenye uwezo mkubwa nchini humo.

Mbali na Dladla, Yanga pia imemtambulisha Kagisho Dikgacoi kama mtaalamu wa mipira ya adhabu na kona (set pieces), eneo ambalo timu hiyo imekuwa ikihitaji maboresho.

Dikgacoi ni kiungo wa zamani wa kimataifa wa Afrika Kusini aliyewahi kucheza katika vilabu vya Golden Arrows, Fulham, Crystal Palace na Cardiff City, huku pia akiichezea timu ya taifa ya Afrika Kusini mara 54 na kufunga mabao mawili.

Alikuwa sehemu ya kikosi cha Afrika Kusini kilichoshiriki Kombe la Dunia 2010, na pia aliisaidia Crystal Palace kupanda kutoka Championship hadi Ligi Kuu ya England msimu wa 2012/13.

Baada ya kustaafu soka mwaka 2018, Dikgacoi alielekeza nguvu zake kwenye ukocha na amekuwa sehemu ya benchi la ufundi la Golden Arrows kabla ya kutua Yanga.

Yanga inaamini ujio wa Dikgacoi utasaidia kuongeza ufanisi katika mipira iliyokufa, huku Dladla akiongeza nguvu kwenye benchi la ufundi katika harakati za kutetea mataji ya ndani na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.

Leave a Comment