
Muigizaji wa filamu nchini, Irene Uwoya, amesema hajawahi kufunga ndoa na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Dogo Janja, akisisitiza kuwa ndoa pekee aliyowahi kuwa nayo ni ile ya aliyekuwa mume wake, marehemu Ndikumana.
Akizungumza katika kipindi cha A List, Uwoya alikanusha taarifa ambazo zimekuwa zikienea kwa miaka kadhaa zikidai kuwa aliwahi kufunga ndoa na Dogo Janja.
“Sijawahi kuwa na ndoa mbili, nina ndoa moja ya marehemu Ndikumana. Sikuolewa na Dogo Janja,” amesema Uwoya.
Kauli hiyo imezua mjadala kutokana na kumbukumbu za mwaka 2017, ambapo Dogo Janja alitangaza hadharani kuwa alimwoa Irene Uwoya.

Mnamo Novemba 3, 2017, akiwa kwenye kipindi cha Leo Tena cha Clouds FM, Dogo Janja, ambaye jina lake halisi ni Abdulaziz Chende, alikiri kuwa walifunga ndoa Oktoba 28, 2017. Alidai kuwa kabla ya ndoa hiyo, Uwoya alisilimu na kupewa jina la Sheillah, huku akieleza kuwa taratibu za posa, mahari na ndoa zilifanyika ndani ya kipindi cha wiki tatu kwa baraka za ndugu wa pande zote.
Katika mahojiano hayo, Dogo Janja, akisaidiwa na mwanamuziki Keisha, alisema walimchukua bibi harusi na kufunga ndoa katika eneo ambalo hawakutaka kulitaja hadharani, baada ya mtangazaji Husna Abdul maarufu Da Huu kuhoji mahali ilikofanyika.
Baada ya uhusiano wao kuvunjika, Irene Uwoya naye aliwahi kuzungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda, ambapo alisema hakuwa amepewa talaka na Dogo Janja licha ya kutokuwa wanaishi pamoja.
“Sijapewa talaka na Dogo Janja na sijawahi kuacha kumpenda hata siku moja, lakini maisha mengine lazima yaendelee na ndiyo maana nikasema sasa hivi niko bize kufanikisha ndoto zangu nyingi nilizokuwa nimejiwekea kwa muda mrefu. Mambo hayo ya kuolewa niwaachie wengine,” alinukuliwa akisema wakati huo.
Kauli mpya ya Uwoya kwamba hakuwahi kufunga ndoa na Dogo Janja sasa imeibua mjadala mpya, ikionekana kutofautiana na simulizi zilizowahi kutolewa hadharani na pande hizo miaka ya nyuma kuhusu uhusiano wao.