
Kipa maarufu wa Mexico, Guillermo Ochoa, ametangaza kustaafu soka la kulipwa baada ya kuweka historia ya zaidi ya miaka 22 akiwa mchezaji wa kulinda lango.
Ochoa mwenye umri wa miaka 41, alithibitisha uamuzi huo kupitia mitandao ya kijamii baada ya kushiriki Kombe la Dunia la sita akiwa na timu ya taifa ya Mexico.
Mchezo wake wa mwisho ulikuwa dhidi ya Jamhuri ya Czech, ambapo aliingia kipindi cha mwisho katika ushindi wa Mexico wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azteca, eneo ambalo alianza rasmi kucheza soka la wakubwa akiwa na Club América mwaka 2004.
Kupitia ujumbe wake, Ochoa alisema:
“Nilitoa kila kitu; niliiacha kila kitu uwanjani kwa klabu zangu na timu ya taifa, na leo nazitundika glavu zangu.”
Kipa huyo aliandika historia kubwa akiwa na Mexico, akishiriki Kombe la Dunia kuanzia Ujerumani 2006, kisha Afrika Kusini 2010, Brazil 2014, Urusi 2018 na Qatar 2022.
Ochoa alikumbukwa zaidi katika Kombe la Dunia 2022 baada ya kuokoa penalti ya mshambuliaji wa Poland, Robert Lewandowski, katika hatua ya makundi.
Katika maisha yake ya klabu, Ochoa aliwahi kucheza katika ligi mbalimbali barani Ulaya zikiwemo Ufaransa, Hispania, Ubelgiji, Italia na Ureno, kabla ya kufunga ukurasa wa safari yake ya soka.