×

Barcelona Yamtambulisha Karim Adeyemi Kuziba Pengo la Lewandowski


Mabingwa wa Ligi Kuu Hispania, Barcelona, wamemtangaza rasmi mshambuliaji Karim Adeyemi baada ya kumsajili kutoka Borussia Dortmund kwa mkataba wa miaka mitano.

Klabu hiyo imesema Adeyemi ataungana tena na kocha Hansi Flick, ambaye ndiye aliyempa nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Barcelona imelipa euro milioni 22 pamoja na nyongeza ya hadi euro milioni 7 kulingana na masharti ya mkataba, huku Borussia Dortmund ikibakiza kipengele cha kunufaika na mauzo yajayo ya mchezaji huyo.

Adeyemi, anayejulikana kwa kasi yake, ana uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa kati au winga. Ameitumikia Borussia Dortmund kwa misimu minne na ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mara 11.

Usajili wake unakuja wakati Barcelona ikifanya maboresho ya safu ya ushambuliaji kufuatia kuondoka kwa mshambuliaji mkongwe Robert Lewandowski, ambaye amejiunga na klabu ya Chicago Fire ya Marekani baada ya kufunga mabao 120 katika misimu minne aliyochezea Barcelona.

Kabla ya usajili wa Adeyemi, Barcelona pia ilikuwa imemsajili winga wa England Anthony Gordon kutoka Newcastle United ili kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu mpya.

Leave a Comment