
Koncept AI Academy imepanua shughuli zake kutoka Tanzania hadi Rwanda kwa kufanikisha AI Masterclass maalum kwa viongozi wa sekta ya ukarimu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuharakisha matumizi ya vitendo ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) barani Afrika.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Kigali yaliwakutanisha wamiliki wa hoteli, mameneja wakuu, wakuu wa idara pamoja na viongozi waandamizi kutoka hoteli mbalimbali nchini Rwanda. Washiriki walijifunza namna AI inavyoweza kuboresha uendeshaji wa biashara za hoteli, kuongeza tija, kuboresha huduma kwa wateja, kukuza mapato na kusaidia kufanya maamuzi ya kimkakati yanayotegemea teknolojia.
Kwa mujibu wa Koncept AI Academy, programu hiyo ni sehemu ya dhamira ya kuwawezesha viongozi, wafanyabiashara, taasisi na serikali za Afrika kupata ujuzi wa vitendo unaohitajika ili kushindana katika uchumi unaozidi kuendeshwa na teknolojia ya AI.

Mbali na mafunzo hayo, ziara ya Academy nchini Rwanda imefungua milango ya ushirikiano wa kimkakati na taasisi mbalimbali ikiwemo Mount Kigali University, Royal FM, Paramount Kigali Hotel pamoja na wadau kutoka Serikali ya Rwanda. Ushirikiano huo unalenga kuimarisha elimu ya AI, mageuzi ya kidijitali, ubunifu na ujenzi wa uwezo wa taasisi nchini humo.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Koncept Group, Dkt. Krantz Mwantepele, amesema dira ya Academy inavuka mipaka ya Tanzania, ikilenga kuifanya Afrika kuwa kitovu cha matumizi na maendeleo ya AI duniani.
“Dira yetu ni kubwa kuliko nchi moja. Tunataka kupeleka elimu ya vitendo ya AI kote Afrika na nje ya bara ili kuwawezesha viongozi, biashara, taasisi na serikali kushindana katika dunia inayoendeshwa na teknolojia ya AI,” alisema Dkt. Mwantepele.

Aliongeza kuwa Afrika haipaswi kubaki kuwa mtumiaji wa teknolojia ya AI pekee, bali inapaswa kuwa sehemu ya viongozi wanaounda mustakabali wa teknolojia hiyo duniani.
Kupitia masterclass za kisekta, mafunzo ya viongozi, programu za kujenga uwezo wa taasisi na ushirikiano wa kimkakati, Koncept AI Academy inalenga kuziba pengo kati ya maendeleo ya teknolojia ya AI na matumizi yake halisi katika sekta mbalimbali.
Academy inaamini kuwa kwa kuwajengea viongozi na taasisi uwezo wa kutumia AI kwa vitendo, Afrika itaongeza tija, kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuandaa kizazi cha viongozi kitakachoongoza zama mpya za teknolojia.
Kwa upanuzi huu nchini Rwanda, Koncept AI Academy imeendelea kuimarisha safari yake ya kujenga jukwaa la Afrika linaloongoza katika elimu ya Akili Mnemba, mageuzi ya kidijitali na maendeleo ya viongozi kwa ajili ya mustakabali wa bara hilo.