×

Mwanamume Ashtakiwa Kwa Mauaji ya EX Wake na Watoto Wawili

Mwanaume mmoja wa jimbo la West Virginia nchini Marekani, Joshua Deel (39), amefunguliwa mashtaka matatu ya mauaji baada ya kudaiwa kumuua aliyekuwa mke wake, Shawn Deel (39), pamoja na watoto wake wawili, Abigale Sloan (18) na Dekota Sloan (16), katika shambulio la kisu lililotokea alfajiri ya Julai 21.

Awali, Joshua alionekana kama mmoja wa waathirika baada ya kupiga simu kwa huduma za dharura akidai kuwa yeye na familia yake walikuwa wameshambuliwa na watu wasiojulikana. Alisema wote walikuwa wamechomwa kwa kisu.

Hata hivyo, maafisa wa polisi walipofika nyumbani hapo walikuta mazingira ya kutisha yakiwa yamejaa damu. Joshua alipatikana sebuleni akiwa amejeruhiwa, huku Shawn na watoto wake wakikutwa katika sehemu tofauti za nyumba wakiwa na majeraha mengi ya visu. Licha ya juhudi za kuwahudumia, wote watatu walitangazwa kufariki.

Uchunguzi wa polisi ulianza kubadili mwelekeo baada ya jirani mmoja kueleza kuwa alisikia mabishano makali kati ya Joshua na mwanamke muda mfupi kabla ya simu ya dharura kupigwa.

Wapelelezi pia walibaini kuwa saa chache kabla ya mauaji hayo, Joshua alidaiwa kunaswa akijaribu kupiga picha za siri za mwanamke mmoja kwa kutumia simu yake, akiipitisha chini ya mlango wa chumba chake bila ridhaa yake. Ingawa awali alikanusha tukio hilo, baadaye alikiri kulifanya na kukubali kuwa kulikuwa na mabishano baada ya kugundulika.

Joshua aliendelea kudai kuwa baadaye usiku alishambuliwa na mtu aliyekuwa amevaa barakoa alipokwenda bafuni, na kwamba alijaribu kuwaokoa waliokuwa ndani ya nyumba lakini hakufanikiwa. Hata hivyo, maelezo hayo yanaendelea kuchunguzwa na polisi.

Silaha inayodhaniwa kutumika katika mauaji hayo ilikutwa kwenye ukumbi wa mbele wa nyumba hiyo.

Kwa sasa, Joshua Deel anashikiliwa bila dhamana huku akikabiliwa na mashtaka matatu ya mauaji ya daraja la kwanza, wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.

Leave a Comment