×

Otamendi Atangaza Kustaafu Soka la Kimataifa Baada ya Miaka 17

Nahodha wa safu ya ulinzi ya Argentina, Nicolas Otamendi, ametangaza kustaafu kuchezea timu ya taifa, akihitimisha safari ya miaka 17 iliyogubikwa na mafanikio makubwa ikiwemo kutwaa Kombe la Dunia 2022 na mataji mawili ya Copa America.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 38 ameichezea Argentina mechi 139 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichofika fainali ya Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani, ambapo walipoteza kwa mabao 1-0 dhidi ya Hispania.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Otamendi amesema uamuzi huo ni mgumu zaidi kuwahi kuandika katika maisha yake ya soka.
“Leo nalazimika kuandika maneno magumu zaidi katika maisha yangu ya soka. Bahati ilivyo, mechi yangu ya mwisho ilikuwa fainali ya Kombe la Dunia.

Hatukupata matokeo tuliyotamani, lakini ninaondoka nikiwa nimeinua kichwa kwa fahari nikijua timu hii ilipambana hadi sekunde ya mwisho.

Asante Argentina kwa kuniruhusu kutimiza ndoto ya kuwa bingwa wa dunia,” ameandika Otamendi.

Baada ya kumaliza miaka 16 ya mafanikio barani Ulaya akizichezea Porto, Valencia, Manchester City na Benfica, Otamendi hivi karibuni alijiunga na miamba ya Argentina, River Plate, ambako ataendelea na maisha yake ya soka katika ngazi ya klabu.

Leave a Comment