
Rais wa Young Africans SC (Yanga), Injinia Hersi Said, amesema msimu wa 2025/26 umekuwa wa mafanikio makubwa kwa klabu hiyo baada ya kutwaa jumla ya makombe manne, huku akiweka bayana mipango ya kuifanya timu kuwa imara zaidi kuelekea msimu wa 2026/27.
Akizungumza na wanachama na mashabiki wa Yanga kupitia Azam TV na Yanga TV, Hersi usiku wa kuamkia leo Julai 25, 2026 alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwapongeza mashabiki wote waliofuatilia tukio hilo, akieleza kuwa lengo lake lilikuwa kutoa tathmini ya msimu uliopita na kueleza dira ya msimu mpya.
Hersi alisema Yanga ilianza msimu kwa mafanikio kwa kutwaa Rayon Cup nchini Rwanda, kabla ya kurejea Tanzania na kushinda Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC. Aidha, timu hiyo iliendeleza ubora wake katika Ligi Kuu ya NBC kwa kutwaa ubingwa baada ya kumaliza msimu kwa ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa mwisho.

Mbali na ubingwa wa ligi, Yanga pia ilitwaa Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, huku safari yake ya Kombe la Shirikisho la CRDB Bank ikiishia hatua ya nusu fainali. Hata hivyo, Hersi alisema mafanikio ya kutwaa makombe manne ndani ya msimu mmoja yanaonyesha uimara na uthabiti wa klabu hiyo.
Rais huyo aliwashukuru wadhamini wote waliounga mkono klabu katika msimu uliopita. Alitoa shukrani maalum kwa GSM kwa mchango wake mkubwa katika uwekezaji na maendeleo ya timu.
Pia aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha sekta ya michezo nchini, huku akimpongeza Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, watendaji wa TFF na Bodi ya Ligi kwa usimamizi wao wa mashindano.

Hersi hakusahau kuwapongeza wanachama na mashabiki wa Yanga kwa sapoti yao isiyoyumba, akisisitiza kuwa mchango wao umekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yaliyopatikana na utaendelea kuwa msingi wa mafanikio makubwa zaidi.
Akihitimisha hotuba yake, Hersi aliwashukuru viongozi wenzake wa Kamati Tendaji wakiongozwa na Makamu wa Rais, Arafat Haji, kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha uongozi.
Aidha, alizungumzia uchaguzi ujao wa klabu, akisema viongozi wote wana wajibu wa kurejea kwa wanachama kuomba ridhaa ya kuendelea kuongoza. Aliwatakia kila la heri wagombea wote na kueleza imani yake kuwa wanachama wa Yanga watawachagua viongozi watakaoendeleza mafanikio ya klabu katika kipindi kijacho.