
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), Moussa Saleh Batraki, jijini Arusha, ambapo wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano na maendeleo ya jumuiya hiyo.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Nchimbi amesisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za OACPS katika kutekeleza mageuzi yatakayoiwezesha taasisi hiyo kuwa imara zaidi na yenye manufaa kwa nchi wanachama.

Aidha, amempongeza Katibu Mkuu wa OACPS kwa hatua anazochukua katika kusukuma mbele ajenda ya mageuzi, ikiwemo kuimarisha uwajibikaji, kuongeza uadilifu na kupunguza utegemezi, hatua ambazo zinalenga kuifanya jumuiya hiyo kuwa na uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu yake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa OACPS, Moussa Saleh Batraki, ameeleza kuwa taasisi hiyo imeweka kipaumbele katika kuimarisha biashara na ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama, pamoja na kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Pia amesema OACPS inalenga kuongeza uwekezaji katika sekta ya TEHAMA, hususan teknolojia za kidijitali, akili unde (Artificial Intelligence), ulinzi na usimamizi wa takwimu pamoja na taarifa. Aidha, imejipanga kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi zinazoendelea na kuwainua wanawake kiuchumi kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya, Jestas Nyamanga, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ellen Maduhu.

