
Watu 35 wamefariki dunia na wengine 30 kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha mabasi mawili kugongana kwenye barabara kuu ya Damascus–Deir Ezzor nchini Syria, Jumamosi.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la kati ya Al-Sukhna na Palmyra, ambapo mabasi hayo yaligongana uso kwa uso.
Kutokana na ukubwa wa ajali hiyo, Wizara ya Ulinzi ya Syria ilituma helikopta kadhaa kuwahamisha majeruhi na miili ya waliofariki kwenda Hospitali ya Kijeshi ya Homs kwa matibabu na utambuzi zaidi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, timu za ambulansi na vyombo vya uokoaji zilifika haraka eneo la tukio na kuanza kuwahudumia majeruhi pamoja na kuondoa miili ya waathirika.
Mkurugenzi wa Idara ya Ambulansi na Dharura katika Wizara ya Afya, Dkt. Najeeb Al-Naasan, amesema hadi sasa idadi ya waliopoteza maisha imefikia 35, huku 30 wakipatiwa matibabu kutokana na majeraha mbalimbali.

Naye Ulinzi wa Kiraia wa Syria umeeleza kuwa ulipeleka vikosi vya uokoaji kutoka kituo cha Palmyra na kuomba msaada wa ziada kutoka vituo vya Deir Ezzor ili kuimarisha operesheni ya uokoaji.
Tukio hilo linakuja siku moja baada ya mamlaka kuripoti kuwa watu 22 walijeruhiwa katika ajali za barabarani na matukio ya moto yaliyotokea maeneo mbalimbali nchini Syria. Aidha, siku ya Alhamisi, mtu mmoja alifariki na wengine 31 kujeruhiwa katika matukio tofauti ya dharura nchini humo.