×

Kipa Maarufu wa Cape Verde Vozinha Akubali Kuhamia Colo Colo

Kipa wa timu ya taifa ya Cape Verde, Vozinha.

SANTIAGO, Chile – Kipa wa timu ya taifa ya Cape Verde, Vozinha, amekubaliana kujiunga na klabu ya Colo Colo ya Chile baada ya kuonyesha kiwango bora katika Kombe la Dunia 2026.

Rais wa Colo Colo, Aníbal Mosa, amethibitisha kuwa mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 40 atatua nchini Chile kwa ajili ya vipimo vya afya kabla ya kutambulishwa rasmi katika uwanja wa Estadio Monumental.

“Vozinha atakuwa mchezaji wa Colo Colo. Katika siku zijazo atasafiri kwenda Chile, atafanya vipimo vya kawaida vya afya kisha atatambulishwa rasmi,” alisema Mosa.

Mosa amesema kiwango cha Vozinha katika Kombe la Dunia ndicho kilichowafanya waamue kumsajili, huku akieleza kuwa usajili huo pia una faida kubwa katika kuongeza mvuto wa kibiashara kwa klabu hiyo.

Vozinha alikuwa miongoni mwa wachezaji waliowashangaza wengi katika michuano ya Kombe la Dunia baada ya kusaidia Cape Verde, timu iliyokuwa ikishiriki kwa mara ya kwanza, kufanya vizuri dhidi ya vigogo wa soka duniani.

Kipa huyo aling’ara baada ya kusaidia Cape Verde kupata sare ya bila kufungana dhidi ya mabingwa watarajiwa wa dunia Hispania, kabla ya kuisukuma Argentina hadi muda wa nyongeza katika hatua ya 32 bora.

Kutokana na kiwango chake, Vozinha alichaguliwa kwenye kikosi bora cha mashabiki cha Kombe la Dunia kilichoandaliwa na FIFA.

Kabla ya Kombe la Dunia, Vozinha alikuwa ametoka kuichezea klabu ya Chaves ya daraja la pili nchini Ureno, akiwa mchezaji huru kabla ya kupata nafasi ya kuendelea na safari yake ya soka nchini Chile.

Leave a Comment