×

JWTZ Yaendelea Kung’ara Katika Operesheni za Kulinda Amani DRC

Kamanda wa Brigedi ya Kujibu Mashambulizi (FIB) chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO), Brigedia Jenerali Alexandar Masangura, ametembelea walinda amani wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wa Kikundi cha Utayari TANZQRF-05 katika eneo la Mambasa, Jimbo la Ituri, mashariki mwa DRC.

Ziara hiyo iliyofanyika Julai 25, 2026, imelenga kujionea mazingira halisi ya kiutendaji na kufuatilia namna kikosi hicho kinavyotekeleza jukumu la kulinda amani katika eneo hilo.

Akiwa huko, Brigedia Jenerali Masangura amewapongeza walinda amani wa Tanzania kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, nidhamu na kujituma licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kimazingira.

Brigedia Jenerali Masangura anaongoza Brigedi ya FIB inayoundwa na vikosi kutoka Tanzania, Malawi, Kenya na Nepal, ambavyo vinafanya operesheni za kulinda raia dhidi ya mashambulizi ya makundi yenye silaha katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Leave a Comment