×

Tetesi za Usajili: Arsenal Yamwania Vinicius Jr, Salah, Zirkzee na Savinho Wabadilisha Mwelekeo

Vilabu vikubwa barani Ulaya vinaendelea kujipanga kuelekea msimu mpya huku tetesi za usajili zikizidi kushika kasi.

Arsenal na Liverpool zimeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Bradley Barcola, lakini mabingwa hao wa Ufaransa wanadaiwa kutaka kiasi cha pauni milioni 145 kwa nyota huyo wa miaka 23.

Kwa upande mwingine, Arsenal bado haijaanza mazungumzo rasmi ya kumsajili winga wa Real Madrid, Vinicius Jr, ingawa miamba hiyo ya Hispania imeweka bei ya euro milioni 160 (takribani pauni milioni 137) iwapo itakubali kumuuza dirisha hili la usajili. Ripoti pia zinaeleza kuwa Arsenal iko tayari kumpa Vinicius mkataba mkubwa zaidi kuwahi kutolewa katika historia ya klabu hiyo. Hata hivyo, kipaumbele cha Mbrazili huyo ni kuongeza mkataba wake na Real Madrid.

Aidha, Arsenal inatajwa kuharakisha mazungumzo ya kumsajili kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes. Kiungo huyo wa Brazil ameripotiwa kuwataka wawakilishi wake kumaliza suala la hatma yake ndani ya wiki moja kabla ya kurejea kambini kwa maandalizi ya msimu mpya.

Kwingineko, Tottenham Hotspur inaongoza mbio za kuwania saini ya winga wa Brazil, Savinho, kutoka Manchester City.

Nayo Real Madrid imefikia makubaliano binafsi na winga chipukizi wa RB Leipzig na Ivory Coast, Yan Diomande, mwenye umri wa miaka 19.

Katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia, Al-Hilal imeanza mazungumzo ya kumsajili winga wa Senegal, Iliman Ndiaye, kutoka Everton.

Chelsea nayo inatarajiwa kudai ada kubwa kwa ajili ya kumuuza winga wa Ureno, Pedro Neto, ambaye anawindwa na Liverpool, Manchester City pamoja na klabu kadhaa za Saudi Arabia.

Nchini Uturuki, Besiktas inasubiri uamuzi wa mshambuliaji wa Misri, Mohamed Salah, baada ya kuwasilisha ofa yake ya mwisho. Salah kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuondoka Liverpool.

Wakati huo huo, Bournemouth imesisitiza kuwa haina mpango wa kumuuza mshambuliaji wake kijana wa Ufaransa, Junior Kroupi, licha ya kuvutiwa na Barcelona.

Kwa upande wa Franco Mastantuono, kiungo wa Argentina mwenye miaka 18, Fulham inaonekana kuwa chaguo kuu ikiwa Real Madrid itaamua kumtoa kwa mkopo msimu ujao.

Nchini Italia, Juventus inaendelea kufanya kazi ya kufanikisha usajili wa mshambuliaji wa Uholanzi, Joshua Zirkzee, kutoka Manchester United.

Hatimaye, kiungo wa Ureno Joao Palhinha anatamani kupigania nafasi yake Bayern Munich, lakini mabingwa hao wa Ujerumani wanadaiwa kuwa tayari kumuuza kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.

Leave a Comment