
Moto mkubwa umezuka katika Shule ya Sekondari Bigwa Sisters, iliyopo Manispaa ya Morogoro, na kuteketeza baadhi ya madarasa, mabweni pamoja na mali za wanafunzi, zikiwemo vitabu, madaftari na vifaa vingine vya kujifunzia.
Akizungumzia tukio hilo, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, DFO Rehema Hamisi, amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha moto huo.
Amebainisha kuwa licha ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na moto huo, hakuna kifo wala majeruhi walioripotiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bigwa Barabarani, Anna Mahinja, amesema tukio hilo limesababisha hofu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, ambao walijitokeza kwa wingi kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika juhudi za kuudhibiti moto na kuzuia usisambae zaidi.
Mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi huku zikifanya tathmini ya kiwango cha hasara iliyosababishwa na tukio hilo.