×

Watu Watatu Wafariki, Wengine Wajeruhiwa katika Ufyatuaji Risasi Seattle

SEATTLE, Marekani – Watu watatu wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya tukio la ufyatuaji risasi kutokea katika tamasha la chakula la Bite of Seattle, lililofanyika karibu na eneo maarufu la Space Needle jijini Seattle, Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi la Seattle, milio ya risasi ilisikiwa majira ya saa 6:01 usiku wa Jumapili, Julai 26, 2026, ambapo maafisa wa polisi walipofika eneo la tukio walikuta watu saba wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi.

Mkuu Msaidizi wa Polisi Seattle, Tyrone Davis, amesema maafisa walitoa huduma ya kwanza mara moja na kuanza juhudi za kuokoa maisha ya wahanga kabla ya kuwapeleka baadhi yao hospitali.

Watu wawili walithibitishwa kufariki eneo la tukio, huku mwingine akifariki baadaye katika Hospitali ya Harborview Medical Center.

Waliofariki wametajwa kuwa ni mwanaume wa miaka 19, mwanaume wa miaka 44 na mwanamke wa miaka 56.

Polisi wamesema mmoja wa majeruhi baadaye alifika katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Washington akiwa na jeraha la risasi. Miongoni mwa waliojeruhiwa ni mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka miwili ambaye hali yake imeelezwa kuwa ni nzuri na thabiti.

Davis amesema uchunguzi wa awali unaonyesha huenda watu wawili walikuwa wakirushiana risasi. Polisi walifanikiwa kumkamata mmoja wa washukiwa, huku mwingine akitoroka na msako ukiendelea.

“Hakuna tishio linaloendelea kwa jamii kwa sasa,” alisema Davis, akiongeza kuwa silaha mbili zimepatikana.

Polisi wameeleza kuwa tukio hilo ni janga kubwa kwa kuwa tamasha la Bite of Seattle limekuwa likifanyika kwa mazingira ya amani bila matatizo makubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Jeshi la Polisi la Seattle liliwataka wananchi kuepuka eneo hilo wakati uchunguzi ukiendelea.

Leave a Comment