×

Video: Dkt. Nshala Ahoji Kesi ya Ugaidi, Asema Inachafua Taswira ya Tanzania

Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Rugemeleza Nshala, amesema chama hicho kina wasiwasi na matumizi ya mashtaka ya ugaidi dhidi ya baadhi ya wananchi na wanachama wake, akidai hali hiyo inaweza kuathiri taswira ya Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 27, 2026, Dkt. Nshala alisema CHADEMA itatoa msaada wa kisheria kwa wanachama na viongozi wake wanaokabiliwa na mashtaka mbalimbali, ikiwemo ya ugaidi.

Aliongeza kuwa timu ya wanasheria wa chama hicho pia itahoji uhalali wa kikatiba wa baadhi ya mashauri yaliyofunguliwa mahakamani.

Dkt. Nshala alisema ni muhimu kujiuliza iwapo kutoa maoni au kukutana kwa madhumuni ya kisiasa kunaweza kutafsiriwa kama ugaidi, huku akisisitiza kuwa CHADEMA haiungi mkono ugaidi kwa namna yoyote.

Alisema chama hicho kinaamini katika matumizi ya njia za amani kufikisha ujumbe wake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan Ibara ya 20(2), pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Aidha, Dkt. Nshala alidai kuwa jumla ya viongozi na wanachama 61 wa CHADEMA wamefunguliwa mashtaka mbalimbali, yakiwemo ya ugaidi. Alisema pamoja na chama hicho kutangaza hadharani kutoshiriki maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Julai 7, 2026, baadhi ya wanachama wake walikamatwa kwa madai ya kuhusika na maandamano hayo.

Kauli hizo zimetolewa na Dkt. Nshala wakati akizungumzia hali ya kisheria inayowakabili baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA waliokamatwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Leave a Comment