
Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imeahirisha hadi Agosti 4, 2026, kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Atlantic Micro Credit Limited, Wendy Ishengoma, na washtakiwa wenzake watatu, baada ya shahidi wa kwanza wa Jamhuri kuhojiwa kwa siku mbili.
Shahidi huyo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Demokrasi Suleiman Livato, alieleza kuwa uchunguzi uliofanywa kufuatia taarifa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ulibaini kampuni hiyo ilikuwa ikikusanya fedha kutoka kwa wananchi bila leseni ya kupokea amana. Pia alidai katika upekuzi wa ofisi za kampuni hiyo zilikamatwa Sh milioni 44.1 pamoja na nyaraka na vifaa mbalimbali.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Madeleka uliendelea kumhoji shahidi huyo kuhusu uchunguzi na vielelezo vilivyowasilishwa, huku Mahakama ikiahirisha shauri hilo hadi Agosti 4, 2026, kwa ajili ya kuendelea na maswali ya utetezi.
Wendy Ishengoma, Sultan Mdee, Frank Tengia na Mwiga Mwiga wanakabiliwa na mashtaka sita, yakiwemo kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa, kuendesha mfumo haramu wa upatu, kufanya biashara ya benki bila leseni na kutakatisha fedha. Jamhuri inadai kampuni hiyo ilikusanya zaidi ya Sh bilioni 5.046 kutoka kwa wateja 2,102 kwa kuwaahidi faida ya asilimia 40 ndani ya siku 25 za kazi.