
Staa wa filamu za Bongo, Irene Uwoya, kupitia ukurasa wake wa insta usiku wa kuamki aleo Julai 27, 2026 ametoa ujumbe wa kugusa hisia akizungumzia changamoto wanazopitia baadhi ya wanaume katika maisha ya kila siku, hasa pale wanapobeba matatizo yao kimya kimya kutokana na shinikizo la kuonekana kuwa wana nguvu kila wakati.
Kupitia ujumbe wake, Irene amesema wapo wanaume ambao hupitia vipindi vigumu, wanabeba majukumu na mawazo mengi lakini hukosa mtu wa karibu wa kuzungumza naye kwa sababu ya kuogopa kuonekana dhaifu.
Amesema hali hiyo inaweza kuwafanya baadhi yao kufikia hatua ya kushindwa kuvumilia, hivyo amewataka wanaume wanaopitia changamoto kutafuta msaada na kushirikisha watu wanaowaamini ili kupata nafuu.

“Unakuta mwanaume anapitia kipindi kigumu, anabeba mambo mengi, anajikaza akisema yeye ni mwanaume, lakini anakosa mtu wa kumshirikisha. Mwisho wa siku anaanguka,” alisema Irene.
Ujumbe huo umepokelewa kwa hisia mbalimbali na mashabiki wake, ambao wamempongeza kwa kuzungumzia suala hilo na kuonyesha uelewa kwa changamoto wanazopitia wanaume.
Baadhi ya mashabiki waliandika:
“Wanawake wanaosikia huruma juu yetu huwa nawaona malaika. Mungu awabariki wanawake wote wanaotupambania,” aliandika mmoja wa mashabiki.
Mwingine alisema: “Ni kama Mwenyezi Mungu kakutumia kulisema hili, na amini kwamba umewagusa wababa wengi.”
Wengine waliendelea kumpongeza Irene kwa kufungua mjadala kuhusu umuhimu wa wanaume kuzungumza na kutafuta msaada wanapokabiliwa na changamoto za maisha.