Diamond na familia yake wakiwa kwenye gari hilo.
WAKATI akiwa kwenye shughuli ya 40 ya mwanayae, Nillan, kipande cha video ya msanii wa muziki wa kizazi kipya Bongo, Diamond Platnumz, inayomuonesha akiwa anaendesha gari kwa mwendo kasi, huku akicheza muziki kiasi cha wakati mwingine kuachia usukani wakati gari likiwa kwenye kasi, kimemtia matatani ambapo sasa ameitwa na Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani kwa ajili ya kuhojiwa.
Katika video hiyo, Diamond akiwa na mzazi mwenzake, Zarina Hassan ‘Zari’, mama yake mzazi, Sanura Kassim ‘Sandra’, Tiffah, watoto wengine na ndugu wa familia hiyo, wanaonekana wakicheza wimbo huo ndani ya gari, wote wakiwa hawajafunga mikanda, jambo ambalo ni hatari na kinyume na sheria ya usalama barabarani.
Kamanda wa Kikosi cha Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema ni kweli amemuita Diamond kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano kwa sababu alichokifanya ni kinyume na sheria za usalama barabarani.
Wakati hayo yakitokea, leo Diamond anafanya sherehe ya arobaini ya mwanaye mchanga, Nillan, shughuli inayofanyikia nyumbani kwake, Madale jijini Dar es Salaam.



