Shirika la Hakimiliki Tanzania (COSOTA) limetoa leseni rasmi kwa Kampuni ya Tanzania Audio Visual Collecting Society (TAVIC) kuwa chombo cha kukusanya na kugawa mirabaha kwa wasanii waliojiunga kama wanachama, hatua inayotarajiwa kuimarisha ulinzi wa haki za wasanii na kuongeza mapato yatokanayo na kazi zao za ubunifu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa COSOTA, Naomi Mungule, amesema utoaji wa leseni hiyo umefanyika baada ya kufuatwa taratibu zote za kisheria, huku akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia wasanii kunufaika zaidi kupitia matumizi ya sauti na video za kazi zao.
Mungule amesema COSOTA inaendelea kuhakikisha mifumo ya usimamizi wa hakimiliki inakuwa imara ili wabunifu wapate stahiki zao kwa wakati na kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa TAVIC, Rajabu Amiry, amesema wasanii wanapaswa kujiunga na TAVIC ili waweze kunufaika na mirabaha inayotokana na matumizi ya kazi zao.
Amesema kampuni hiyo imejipanga kusimamia kwa uwazi ukusanyaji na ugawaji wa mirabaha, huku lengo kuu likiwa kuhakikisha kila msanii anapata haki yake kulingana na matumizi ya kazi zake za ubunifu.
Naye msanii wa filamu nchini, Godliver, amepongeza hatua hiyo akisema mfumo huo ni fursa muhimu kwa wasanii kupata haki zao na kuongeza thamani ya kazi wanazozalisha.
Amesema ushirikiano kati ya COSOTA, TAVIC na wasanii utakuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya ubunifu nchini, huku akiwahimiza wasanii kujisajili ili wawe sehemu ya mfumo mpya wa mirabaha unaolenga kuwanufaisha zaidi.