×

Katambi: Tanzania Haina Ugaidi, Lakini Kuna Viashiria vya Matendo ya Kigaidi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii, akisema baadhi ya maudhui yanayosambazwa yanalenga kupotosha umma.

Akizungumza leo, Julai 29, 2026, visiwani Zanzibar, Waziri Katambi amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kufanya shughuli zao za kila siku, huku akisisitiza kuwa Tanzania ipo salama na Serikali inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda raia pamoja na mali zao.

Katambi amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, huku akisisitiza kuwa Serikali inazingatia misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na uhuru wa mahakama.

“Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama inao wajibu wa msingi wa kulinda haki za raia na mali zao kwa mujibu wa Katiba na sheria mbalimbali. Tunaheshimu utawala wa sheria; sisi ni nchi inayoheshimu demokrasia pamoja na uhuru wa mahakama,” amesema Katambi.

Waziri huyo amesisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria, akieleza kuwa kila anayebainika kuvunja sheria atachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

Amesema mtuhumiwa yeyote atakayekamatwa atafikishwa katika vyombo vya sheria pamoja na ushahidi au vielelezo vitakavyopatikana, ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa.

Akizungumzia suala la ugaidi, Katambi amesema Tanzania haina matukio makubwa ya ugaidi, lakini kuna uwezekano wa kuwepo kwa viashiria vya matendo yanayoweza kuhusishwa na vitendo hivyo.

“Tanzania hatuna ugaidi kwa maana ya matukio makubwa, lakini vinaweza kuwepo viashiria vya matendo ya kigaidi. Ugaidi una vipengele mbalimbali vya makosa na unajumuisha kila aina ya tendo ikiwemo kutishia, kupanga, kuratibu, kula njama, kutekeleza au kuandaa zana zinazoweza kuleta madhara na kuzuia shughuli za kiuchumi,” alisema.

Katambi amewataka wananchi kuwa makini na taarifa zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka husika, huku Serikali ikiendelea kuhakikisha amani na usalama vinaendelea kudumishwa nchini.

Leave a Comment