
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema ndege za kijeshi za Marekani zilitumia baadhi ya vituo vya kijeshi vya Israel wakati wa mashambulizi dhidi ya Iran katika vita vya hivi karibuni.
Katz amesema Iran inafahamu kuhusu ushirikiano huo kati ya Marekani na Israel, lakini hadi sasa haijachukua hatua yoyote ya moja kwa moja dhidi ya Israel kutokana na tukio hilo.
Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha 14 cha Israel, Katz amesema licha ya Iran kufanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati, Israel haijawa miongoni mwa maeneo yaliyolengwa katika kipindi hicho.
“Ukweli ni kwamba kwa sasa Wairan wanashambulia kila mahali katika eneo hili isipokuwa nchi moja: Israel. Ingawa hali hiyo inaweza kubadilika ndani ya saa moja,” alisema Katz.
Kauli hiyo imetolewa wakati Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akiwa mjini Washington kwa mazungumzo na Rais wa Marekani, Donald Trump, ambapo masuala ya Iran, usalama wa Mashariki ya Kati na migogoro ya kikanda yanatarajiwa kuwa sehemu ya ajenda kuu.
Katz ameonya kuwa Israel haitasita kujibu kwa nguvu endapo itafanyiwa shambulio na Iran, akisema tayari serikali ya Israel imeweka wazi msimamo wake kuhusu ulinzi wa taifa hilo.
“Mimi na Waziri Mkuu tulitangaza wazi kwamba iwapo Israel itashambuliwa, tutajibu kwa nguvu zote,” alisema.
Mvutano kati ya Israel na Iran umeendelea kuwa miongoni mwa masuala yanayofuatiliwa kwa karibu duniani, huku Marekani ikiwa mshirika mkubwa wa Israel katika masuala ya usalama na kijeshi.