TEHRAN: Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi makubwa dhidi ya Iran siku ya Alhamisi, likisema ni hatua ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya Iran yaliyolenga vituo vya jeshi la Marekani nchini Jordan. Hatua hiyo imefufua mapigano katika Mashariki ya Kati na kuzidisha mvutano uliokuwa umetulia kwa takribani wiki moja.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema mashambulizi hayo ni “jibu lenye nguvu” kwa kile ilichodai kuwa ni mashambulizi ya Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani walioko katika eneo hilo.
Mashambulizi hayo yamezima matumaini ya kurejea kwenye mazungumzo ya kidiplomasia yaliyokuwa yakitarajiwa baada ya kipindi kifupi cha utulivu.
Rais wa Marekani, Donald Trump, alinukuliwa na Fox News akisema kabla ya operesheni hiyo kuwa, “Tutawashambulia kwa nguvu… tutawashinda vibaya.”
Kwa upande wake, televisheni ya taifa ya Iran iliripoti kuwa eneo la mpakani la Piranshahr lilishambuliwa na Marekani, huku shirika la habari la Fars likisema kombora lilipiga eneo lisilo na wakazi na halikusababisha vifo.

Jeshi la Jordan lilitangaza kuwa lilifanikiwa kuzuia makombora matano yaliyokuwa yamerushwa na Iran, wakati Walinzi wa Mapinduzi wa Iran (IRGC) wakidai kuwa walilenga vituo vya Marekani nchini humo.
IRGC ilisema itaendelea na kile ilichokiita harakati za upinzani mradi vitisho dhidi ya Iran vitaendelea.
Wakati huo huo, Israel imeishutumu Hezbollah kwa kutuma ndege isiyo na rubani (drone) iliyolenga gari la Israel ndani ya Lebanon, ikidai hatua hiyo imekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Katika upande mwingine wa mzozo, Marekani na Saudi Arabia zilifanya mashambulizi ya pamoja dhidi ya maeneo ya wanamgambo nchini Iraq wanaodaiwa kuungwa mkono na Iran. Jeshi la Marekani lilisema lililenga maghala ya silaha na vituo vya vifaa vya kijeshi vya kundi hilo

Muungano wa Hashed Al-Shaabi ulidai watu wasiopungua 20 waliuawa katika mashambulizi hayo, huku ukiyataja kuwa ni “hatua hatari ya uchokozi.” Maafisa wa kundi hilo pia walidai washauri watano wa kijeshi kutoka Iran walikuwa miongoni mwa waliouawa.
Serikali ya Iraq ililaani mashambulizi hayo na kusisitiza kuwa haitakubali ukiukwaji wa mamlaka yake, ikisema itachukua hatua dhidi ya yeyote atakayetumia ardhi yake kuhatarisha usalama wa nchi jirani.
Mvutano huo pia umeathiri usafirishaji wa mafuta duniani. Iran imedai kuwa imezuia meli tatu za mafuta katika Mlango wa Hormuz na kusisitiza kuwa ina udhibiti kamili wa njia hiyo muhimu ya biashara ya nishati. Aidha, Tehran imetangaza mpango wa kutoza ada kwa meli zinazopita katika mlango huo, jambo ambalo Marekani inapinga.
Kutokana na hali hiyo, umuhimu wa Bahari ya Shamu umeongezeka kama njia mbadala ya kusafirisha mafuta kutoka Saudi Arabia kwenda masoko ya kimataifa. Marekani pia imetangaza vikwazo vipya dhidi ya taasisi zinazohusishwa na Walinzi wa Mapinduzi wa Iran, ikizituhumu kwa kulazimisha meli zinazopita katika Mlango wa Hormuz kulipa tozo.