
Kikosi cha Yanga kinaendelea na maandalizi makali ya msimu mpya katika kambi ya Avic Town, Kigamboni, Dar es Salaam, huku benchi jipya la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu Manqoba Mngqithi likianza kuijenga timu kuelekea msimu wa 2026/27.
Mazoezi hayo yamekuwa na kasi na ushindani mkubwa, huku wachezaji wakionyesha ari ya juu chini ya programu mpya ya benchi la ufundi, ambalo lina dhamira ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa.

Miongoni mwa nyota wapya walioanza kujifua kambini ni mshambuliaji kutoka Senegal Cheikh Ibrahima Touré, winga wa Zambia Albert Deddo Kangwanda Jr, pamoja na mshambuliaji/winga wa Comoro Housseine Zakouani, ambao wanaendelea kuzoea mfumo wa kocha Mngqithi.
Mbali na nyota hao wapya, wachezaji wengine wa kikosi hicho wanaendelea na mazoezi ya nguvu yanayojumuisha utimamu wa mwili, mbinu za kiufundi na mifumo ya uchezaji, huku benchi la ufundi likitumia kipindi hiki kuunda kikosi kitakachokuwa na ushindani mkubwa msimu ujao.

Mshambuliaji mpya wa Namibia Peter Shalulile, ambaye ametangazwa rasmi kujiunga na Yanga, bado hajaripoti kambini kuanza mazoezi na wenzake.
Mashabiki wa Yanga wameendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kambi hiyo wakiamini usajili mpya pamoja na benchi jipya la ufundi vitaiwezesha timu kuendelea kufanya vizuri ndani na nje ya Tanzania.



