
Msanii wa muziki wa rap kutoka Marekani, Cardi B, ameamua kuachia rasmi wimbo wake mpya unaoitwa “Ah Ha” baada ya kipande kifupi cha wimbo huo kuzua gumzo kubwa mitandaoni na mashabiki kumtaka autoe haraka.
Cardi B alitoa kipande cha wimbo huo kwa mara ya kwanza kwenye mitandao yake ya kijamii akiwa ufukweni, akionekana kuvaa bikini yenye bendera ya Jamhuri ya Dominika huku akiimba sehemu ya wimbo huo.
Katika chapisho hilo aliandika ujumbe mfupi, “Hmmmmm… why not?”, jambo lililoamsha hisia za mashabiki wake wengi duniani.
Baada ya kipande hicho kusambaa kwa kasi, mashabiki walimiminika kwenye mitandao wakimtaka msanii huyo kuachia wimbo huo mara moja.
Mmoja wa mashabiki aliandika: “Nipe huu wimbo sasa hivi, siwezi kusubiri,” huku mwingine akisema kuwa wimbo huo una sauti mpya na unahitaji kutolewa rasmi haraka.
Cardi B baadaye alieleza kuwa awali hakuwa na mpango wa kutoa wimbo huo kwa wakati huu, lakini mwitikio mkubwa wa mashabiki ulimfanya abadili uamuzi.
Kupitia mazungumzo yake kwenye Instagram Live, alisema yeye na lebo yake ya muziki walishangazwa na mapokezi hayo na sasa walilazimika kuharakisha maandalizi ya video ya muziki.
“Niliona jinsi mlivyopenda, sasa nahisi natakiwa kurekodi video ya muziki mwishoni mwa wiki,” alisema Cardi B.
Wimbo huo unatarajiwa kutoka rasmi Ijumaa, Julai 31, 2026, kupitia lebo yake ya Atlantic Records.