
Dar es Salaam – Mahakama ya Rufani ya Tanzania imetupilia mbali shauri la marejeo Na. 720316/2026 lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, likitaka kupitiwa mwenendo na uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Februari 24, 2026 katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Marejeo hayo yaliwasilishwa kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kukataa kupokea ushahidi wa ziada kutoka kwa ACP Amini Mahamba, ambaye alikuwa Mpelelezi Mkuu wa matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Katika uamuzi uliotolewa Julai 30, 2026 na jopo la Majaji wa Rufani Mwarija, Muruke na Khamis, mahakama ilieleza kuwa Mahakama Kuu ilitafsiri kwa usahihi Kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Majaji hao walibainisha kuwa kifungu hicho kinahusu ushahidi wa shahidi ambaye hakuwahi kutajwa wala kusomewa ushahidi wake wakati wa mwenendo wa awali wa kupeleka shauri Mahakama Kuu (committal proceedings), na si shahidi ambaye tayari ushahidi wake uliwasilishwa na baadaye kuongezewa ushahidi mpya.
“Katika mazingira hayo, tunakubaliana na mahakama ya awali kwamba Kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinamhusu shahidi ambaye hakutajwa wala ushahidi wake kusomwa kwa mshtakiwa wakati wa mwenendo wa awali wa kupeleka shauri Mahakama Kuu (committal proceedings),” sehemu ya uamuzi huo imeeleza.
Mahakama iliongeza kuwa notisi iliyowasilishwa na DPP haikuwa na msingi sahihi wa kisheria, hivyo Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kuifuta.
“Kwa kuzingatia sababu zilizotangulia, tunaona kuwa notisi hiyo ilikuwa imewasilishwa kwa msingi usio sahihi wa kisheria (misconceived), na hivyo mahakama ya awali ilikuwa sahihi na ilijielekeza ipasavyo kuifuta (strike out),” umeeleza uamuzi huo.
Februari 22, 2026, upande wa Jamhuri uliwasilisha notisi ya ushahidi wa ziada wa ACP Mahamba kuhusu ripoti ya matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi. Hata hivyo, Lissu alipinga hatua hiyo akidai ilikuwa kinyume na sheria, hoja ambayo Mahakama Kuu iliikubali.
Wakati huo huo, Mahakama ya Rufani imekataa ombi la Lissu la kutaka alipwe fidia kutoka kwa DPP kwa madai ya kusababishiwa usumbufu kwa siku 139. Mahakama ilieleza kuwa haina mamlaka ya kuamua suala hilo katika hatua ya sasa kwa kuwa kesi ya msingi bado inaendelea na haijafikia tamati.