×

Kijana wa Miaka 16 Aokoa Mtoto Baharini, Aibuka Shujaa wa Taifa Marekani,

Kijana mwenye umri wa miaka 16, Ryder Williams, ambaye amesifiwa kama shujaa wa kitaifa nchini Marekani baada ya kuokoa mtoto wa miaka 10 aliyekuwa akizama katika ufukwe wa California, amezungumza kwa mara ya kwanza tangu tukio hilo kutokea.

Williams, ambaye ni mlinzi wa bahari (lifeguard) wa mwaka wake wa kwanza katika California State Parks, alikuwa akifanya kazi katika mnara wa ulinzi namba 2 kwenye ufukwe wa Seabright State Beach wakati alipogundua mtoto huyo, Nathaniel Rai, akisombwa na mawimbi makubwa.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Williams aliona mtoto huyo akipoteza mwelekeo kwenye maji ya kina kifupi kabla ya kusukumwa ghafla kuelekea eneo lenye maji marefu na mawimbi yenye nguvu.

“Nilitoa taarifa kwa redio, nikaiweka pembeni pamoja na miwani yangu, kisha nikakimbia kuelekea kwa mtoto,” Williams alisema akielezea tukio hilo.

Alisema aliingia majini haraka akiwa na vifaa vyake vya uokoaji, lakini kutokana na nguvu ya mawimbi hakuweza kutumia njia ya kawaida ya kumvuta mtoto huyo. Alisema mtoto huyo alianza kulegea wakati mawimbi yakipiga juu yao.

“Nilikuwa sitamuachia. Nilijua alikuwa katika hatari kubwa na sikutaka hilo litokee,” alisema Williams.

Katika uokoaji huo uliodumu zaidi ya dakika mbili, lifeguard mwenzake Aaron Bohnen pamoja na baadhi ya watu waliokuwa ufukweni walijitokeza kusaidia. Baada ya kumfikisha mtoto huyo salama ufukweni, Williams alichukua vifaa vya huduma ya kwanza na mtoto huyo akakaguliwa na wahudumu wa afya kabla ya kuunganishwa tena na familia yake.

“Nashukuru kupata nafasi ya kumrudisha mtoto huyo kwa familia yake akiwa salama. Hii ndiyo kazi yangu na ninaipenda,” alisema kijana huyo.

Tukio hilo lilimfanya Williams kualikwa katika Ikulu ya Marekani na Rais Donald Trump kwa ajili ya kupokea heshima maalum ya kiraia.

Mtu aliyerekodi video ya tukio hilo, Scott Vander Dussen, alisema bila msaada wa Williams huenda mtoto huyo asingesalimika.

“Ilitokea kwa haraka sana. Mtoto alizidiwa na mawimbi na kusombwa ndani ya muda mfupi,” alisema Vander Dussen akizungumza na NBC.

Ujasiri wa Williams umeendelea kusifiwa kama mfano wa kujitolea na umuhimu wa kuwa na walinzi wenye mafunzo katika maeneo yenye hatari ya maji.

Leave a Comment