
Wanachama wa Yanga leo Agosti 2, 2026 wamewapitisha Eng. Hersi Said kuwa Rais na Arafat Haji kuwa Makamu wa Rais wa klabu hiyo kwa kipindi kingine cha miaka minne, katika Uchaguzi Mkuu wa Yanga wa mwaka 2026.
Akizungumza mbele ya wanachama, Eng. Hersi Said alieleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake katika kipindi cha miaka minne iliyopita, akisema Yanga imeandika historia mpya ndani na nje ya uwanja.
Alisema katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imecheza mechi 120, ikishinda 101, sare 12 na kupoteza mechi saba pekee. Klabu hiyo imekusanya pointi 315, kufunga mabao 286 na kuruhusu mabao 51 tu, ikiwa na tofauti ya mabao 235.
Katika Kombe la Shirikisho la CRDB (CRDB Federation Cup), Hersi alisema Yanga imeweka rekodi ya kutwaa taji hilo mara nne mfululizo, huku ikipevuka bila kupoteza mchezo hata mmoja katika mechi 28 ilizocheza kwa kipindi cha miaka mitano. Katika mashindano hayo, Yanga imefunga mabao 86, kuruhusu mabao 14 na kuweka rekodi ya clean sheet 20.
Mbali na mafanikio hayo, Hersi alisema Yanga imefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii mara nne, pamoja na kushinda Toyota Cup nchini Afrika Kusini baada ya kuifunga Kaizer Chiefs mabao 4-0, na baadaye kutwaa Rayon Day Cup nchini Rwanda kwa kuichapa Rayon Sports mabao 3-1.
Hersi aliwatumia salamu viongozi wenzake waliomaliza muda wao wa uongozi na kuwapongeza kwa ushirikiano waliouonyesha.
“Niwapongeze viongozi wote ambao tumefanya kazi pamoja. Niwatakie kila la heri kwenye uchaguzi. Nitafurahi kama mtarudi wote, lakini natambua pia kuwa kuna wanachama wengine wenye uwezo wa kuongoza. Kama yupo mgombea mnayeona anafaa, mchagueni. Mimi nipo tayari kufanya kazi na mwanachama yeyote mwenye dhamira njema kwa klabu yetu,” alisema Hersi Said.
Kupitishwa kwa Hersi Said na Arafat Haji kunawapa nafasi ya kuendelea kuiongoza Yanga kwa muhula mwingine wa miaka minne, huku wanachama wakitarajia kuona klabu ikiendeleza mafanikio yake ndani na nje ya Tanzania.