
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu leo Agosti 3, 2026 amesema alifanya jitihada za kuitisha mkutano wa dharura kufuatia maelekezo aliyoyapokea kutoka Serikalini, lakini akajulishwa kuwa tarehe aliyopendekeza kulikuwa na shughuli ya marathon.
Akizungumza katika kipindi cha redio cha Crown Sport, Mangungu alisema yeye ndiye Mwenyekiti halali wa Simba SC aliyechaguliwa na wanachama, huku akieleza kuwa mabadiliko yanayofanyika ndani ya klabu yanapaswa kuzingatia matakwa ya kisheria na kufanywa na wanachama wenyewe.
“Mimi ndiye Mwenyekiti wa Simba SC kwa kuchaguliwa na wanaofanya mabadiliko ni wanachama wa Simba SC na yapo matakwa kisheria yanayowalazimu kufanya hayo mabadiliko,” alisema.
Mangungu alifafanua kuwa alipokea barua kutoka Serikalini kuhusu suala hilo na kuiwasilisha kwa wajumbe wote wa Bodi kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi.
Baadaye aliandika tena barua akieleza nia ya kufanya mkutano wa dharura tarehe 2 Agosti, lakini akapatiwa majibu kuwa siku hiyo kulikuwa na mpango wa kuendesha marathon.
“Mkutano wa dharura una utaratibu wake wa kuitishwa. Nilipokea barua kutoka Serikalini na nilivyopokea niliiwasilisha kwa wajumbe wote wa Bodi kupitia kwa Mwenyekiti.
Baadaye nikamwandikia tena barua nikamwambia kutokana na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali nategemea kufanya mkutano Agosti 2, akanijibu tarehe hiyo tunakusudia kufanya marathon,” alisema Mangungu.