
Arusha, Agosti 4, 2026 – Airtel Tanzania imeendelea kuimarisha uhusiano wake na wateja pamoja na wadau wa biashara kupitia mashindano ya Airtel Business Monthly Mug Tournament yaliyofanyika katika Klabu ya Gymkhana jijini Arusha.
Mashindano hayo yaliwakutanisha viongozi wa biashara, wateja na wadau mbalimbali, yakitoa jukwaa la kujenga mahusiano ya karibu, kubadilishana uzoefu na mawazo, pamoja na kutambua fursa mpya za kukuza biashara. Aidha, tukio hilo lilitumika kuonyesha dhamira ya Airtel ya kuunga mkono maendeleo ya mchezo wa gofu nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Airtel Business, Joseph Vipond, alisema kampuni hiyo inaamini kuwa ushirikiano imara hujengwa kupitia mawasiliano ya karibu na ushiriki endelevu, huku michezo ikiwa njia muhimu ya kuimarisha mahusiano hayo.

“Nje ya mazingira ya kawaida ya kikazi, wadau wanapata nafasi ya kuzungumza, kujenga uaminifu na kushirikiana katika kutafuta fursa mpya za maendeleo ya biashara,” alisema Vipond.
Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano kwa Umma wa Airtel Tanzania, Sarah Nassor, alisema mashindano hayo yanaakisi dhamira ya kampuni ya kujenga mahusiano ya muda mrefu na wadau wake kwa kuwashirikisha katika shughuli zinazokuza mawasiliano, uaminifu na ushirikiano.

Mmoja wa wateja wa Airtel, Hiten Nathwani, aliipongeza kampuni hiyo kwa kuendelea kuboresha huduma zake huku akiwahamasisha wachezaji wa gofu na wadau wengine kutumia huduma za Airtel kwa mawasiliano na biashara zao.
Kupitia Airtel Business Monthly Mug Tournament, Airtel Tanzania inaendelea kuthibitisha kuwa ushirikiano wa kweli hauishii kwenye huduma za biashara pekee, bali unajengwa kwa kuwaleta pamoja watu kutoka sekta mbalimbali, kuimarisha mahusiano na kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi wa kidijitali nchini.