
Mwimbaji maarufu wa Marekani, Ariana Grande, anatarajiwa kupunguza shughuli zake za kikazi na kuonekana hadharani baada ya kukamilisha ziara yake ya muziki ya Eternal Sunshine mwezi ujao.
Kwa mujibu wa mwakilishi wake aliyenukuliwa na jarida la People, Ariana, mwenye umri wa miaka 33, ameamua kuchukua mapumziko kutoka kwenye shughuli zinazomweka kwenye macho ya umma kufuatia uchunguzi na mijadala ya muda mrefu kuhusu maisha yake binafsi na muonekano wake.
Uamuzi huo pia umeathiri ushiriki wake katika tamasha la muziki Sunday in the Park with George, ambalo linatarajiwa kuonyeshwa katika ukumbi wa Barbican jijini London mwaka 2027.

Waandaaji wa onyesho hilo wamethibitisha kuwa Grande hataendelea na nafasi hiyo na wameeleza kuwa wanaunga mkono uamuzi wake.
Katika miaka ya hivi karibuni, Ariana amekuwa akizungumziwa sana kwenye mitandao ya kijamii kuhusu afya yake na muonekano wa mwili wake. Mjadala huo uliongezeka zaidi baada ya kuachia albamu yake mpya, Petal, na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kuitangaza.
Mwakilishi wake amesema mwimbaji huyo analenga kumaliza ziara ya Eternal Sunshine akiwa na mafanikio makubwa, afya njema na furaha, kabla ya kuchukua muda wa kupumzika mbali na ratiba nzito ya kazi.
Ariana Grande ni miongoni mwa wasanii wakubwa duniani, akiwa amejijengea umaarufu kupitia nyimbo zilizofanya vizuri kimataifa kama Thank U, Next, 7 Rings na Positions. Mbali na muziki, pia amefanikiwa katika tasnia ya uigizaji na kuendelea kujizolea mashabiki duniani kote.