Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ni miongoni mwa taasisi za sekta binafsi zilizotia saini Tamko la Pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, katika hafla iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Kwa niaba ya TWCC, Tamko hilo lilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Dkt. Mwajuma Hamza, ambaye pia aliwasilisha salamu za wanawake wafanyabiashara nchini, akisisitiza utayari wao kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia biashara, uwekezaji, ubunifu na ujasiriamali ili kuchochea ukuaji wa uchumi shindani, jumuishi na endelevu.

Tamko hilo linaweka msingi wa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, likilenga kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, kutatua changamoto zinazoikabili sekta binafsi, na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Kupitia ushiriki huo, TWCC imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kushirikiana na Serikali katika kujenga mazingira wezeshi ya biashara na kuhakikisha wanawake wafanyabiashara wanakuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na maendeleo endelevu ya Tanzania.