×

Mkurugenzi wa Stanbic Bank Tanzania Kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Miundombinu Afrika

Dar es Salaam, Agosti 4, 2026 – Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira, anatarajiwa kuungana na viongozi wa kimataifa, mawaziri, watunga sera, wawekezaji, taasisi za fedha za maendeleo na viongozi wa sekta binafsi katika Mkutano wa Infra for Africa Forum 2026, utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 5 hadi 6.

Mkutano huo umeandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano na Africa50, ukiwa na lengo la kujadili mbinu bunifu za kuharakisha maendeleo ya miundombinu na kuongeza uwekezaji barani Afrika. Mgeni rasmi wa mkutano huo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika siku ya kwanza ya mkutano, Agosti 5, Rwegasira atashiriki katika mjadala wa ngazi ya juu wenye mada “Reinvesting for Expansion: Asset Recycling as a Multiplier”, ambapo atakuwa pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Nishati na Miundombinu Duniani wa Standard Bank Group, Dele Kuti, na viongozi wengine waandamizi.

Katika mjadala huo, viongozi hao watajadili masuala ya ugharamiaji wa miradi ya miundombinu, uhamasishaji wa mitaji pamoja na umuhimu wa ushirikiano wa kimkakati katika kuharakisha uwekezaji wa miundombinu barani Afrika.

Siku inayofuata, Agosti 6, Rwegasira atakuwa miongoni mwa wazungumzaji katika kikao cha jumla chenye mada “Pace Setters: African-Designed, African-Led”, kitakachowakutanisha viongozi kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Ecobank, ATIDI pamoja na Mfuko wa Uwekezaji wa Taifa wa Angola.

Kikao hicho kitajadili namna taasisi za kifedha za Afrika, benki, wawekezaji wa kitaifa na wadau wa miundombinu wanavyoweza kuhamasisha mitaji ya ndani, kuimarisha mifumo ya kupunguza hatari za uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi kupitia suluhu zinazoandaliwa na kuongozwa na Waafrika.

Ushiriki wa Stanbic Bank Tanzania katika mkutano huo unaonyesha dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kuchangia mijadala na suluhisho za kifedha zinazolenga kukuza uwekezaji wa miundombinu, maendeleo ya uchumi na ushirikiano wa kikanda barani Afrika.

Leave a Comment