×

UEFA Kuchukua Hatua Dhidi ya Mpango wa FIFA wa Kuuza Hisa za Kombe la Dunia

Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) limetishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mpango uliokuwa ukipendekezwa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino, wa kuuza sehemu ya hisa katika mashindano ya FIFA kwa wawekezaji binafsi.

UEFA imeeleza kuwa inazingatia kutumia njia za kisheria, usuluhishi au malalamiko ya kikanuni kutokana na mpango huo ambao ulilenga kuanzisha kampuni tanzu ya kibiashara itakayokuwa ikisimamia matukio makubwa ya FIFA ikiwemo Kombe la Dunia.

Kupitia mpango huo, FIFA ilipanga kuanzisha kampuni mpya iitwayo FIFA Forward Enterprise (FFE) ambayo ingeweza kupokea uwekezaji kutoka kwa wadau wa nje kwa kununua hisa ndogo zisizokuwa na mamlaka ya udhibiti.

Hata hivyo, mpango huo umekumbana na upinzani kutoka kwa mashirikisho mbalimbali ya soka duniani, yakiwemo UEFA pamoja na mashirikisho ya Amerika Kaskazini, Kati na Karibea (Concacaf), ambayo yameonyesha kutoridhishwa na hatua hiyo.

UEFA katika barua yake kwa Infantino imeeleza kuwa inaona kuna sababu za kuchukua hatua za kisheria kutokana na mpango wa FFE, huku ikimtaka uongozi wa FIFA kuhakikisha nyaraka na taarifa zote zinazohusiana na mpango huo zinahifadhiwa.

Wakati huo huo, Chama cha Soka cha England (FA) kinatarajiwa kumwandikia Infantino barua ya kuondoa uungaji mkono wake wa awali kwa azma yake ya kuendelea kuongoza FIFA.

Nchi ya Wales tayari imekuwa taifa la kwanza kutangaza hadharani kuondoa uungaji mkono wake kwa Infantino baada ya kuibuka kwa mjadala kuhusu mwelekeo wa uongozi wa FIFA.

FIFA imekuwa ikitetea mpango huo ikisema uwekezaji huo ungekuwa na lengo la kuongeza mapato na kukuza thamani ya mashindano yake, huku ikisisitiza kuwa wawekezaji hao wasingekuwa na uwezo wa kuingilia maamuzi ya uendeshaji wa soka.

Hata hivyo, wapinzani wa mpango huo wana wasiwasi kuwa hatua hiyo inaweza kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa mashindano makubwa ya FIFA na kuipa nafasi kubwa sekta binafsi katika maamuzi ya kibiashara ya soka duniani.

Leave a Comment