×

Depú Akaribia Kuachana na Yanga? Petro de Luanda Yajitokeza

DAR ES SALAAM: Klabu ya Yanga SC imemweka sokoni mshambuliaji wake wa kimataifa wa Angola, Laurindo Dilson Maria Aurélio maarufu kama Depú, baada ya kufanya maboresho katika safu yake ya ushambuliaji.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Yanga SC kuingiza mastraika wawili wapya wa kimataifa kwenye kikosi chake, jambo lililoifanya klabu hiyo kuona kuna umuhimu wa kumpa nafasi Depú kutafuta changamoto nyingine nje ya Jangwani.

Depú, ambaye alisajiliwa kutoka Angola, sasa anaweza kuondoka endapo kutapatikana klabu itakayofikia makubaliano na Yanga kuhusu ada ya uhamisho.

Klabu yake ya zamani ya Petro de Luanda imeonyesha nia ya kumrejesha mshambuliaji huyo nchini Angola, lakini mazungumzo kati ya pande hizo bado hayajafikia mwafaka.

Yanga imeweka dau la dola za Marekani 500,000 kama thamani ya kumuuza Depú, kiasi ambacho Petro de Luanda inakiona kuwa ni kikubwa kwa uwezo wao kwa sasa.

Hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa kati ya Yanga na Petro de Luanda, huku hatma ya mshambuliaji huyo wa Angola ikiwa bado haijajulikana.

Depú anakuwa miongoni mwa wachezaji ambao mustakabali wao unatajwa zaidi katika dirisha hili la usajili, huku Yanga ikiendelea kupanga kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya.

Leave a Comment