
Tetesi zinazomhusisha kiungo wa Azam FC, Feisal Salum “Fei Toto”, na usajili wa Yanga au Simba zimeendelea kutawala mijadala ya soka nchini, huku jezi yenye namba 6 ikigeuka kuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa watani hao.
Mjadala huo ulipata nguvu baada ya mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji (Mo Dewji), kuchapisha kwenye Insta Story yake picha ya jezi ya Simba yenye namba 6 mgongoni. Muda mfupi baadaye, Yanga nao walichapisha picha yenye namba hiyo kwenye kurasa zao rasmi, hatua iliyozua tafsiri mbalimbali kutoka kwa mashabiki waliodhani huenda kulikuwa na ujumbe maalumu kuhusu Fei Toto.
Mbali na picha hizo, kauli za Afisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, zimeendelea kuchochea mjadala. Katika Mkutano Mkuu wa Yanga uliofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam, Kamwe aliwaambia wajumbe kuwa mtu aliyekuwa akisumbua klabu hiyo alikuwa GSM kashamalizana na GSM.
Si hilo tu. Wakati kikosi cha Yanga kikisafiri kuelekea Geita, Kamwe pia alisema kuwa kulikuwa na watu wanaendelea kufanya mazoezi na mchezaji ambaye ni mali ya Yanga. Kauli hiyo ilitafsiriwa kwa njia tofauti na mashabiki na kuongeza uzito wa tetesi za usajili.
Wakati mashabiki wa Simba na Yanga wakiendelea kurushiana vijembe kuhusu hatima ya Fei Toto, Azam FC bado haijatoa tamko lolote kuhusu uvumi huo. Badala yake, leo Agosti 5, 2026, klabu hiyo imezindua jezi zake mpya za msimu wa 2026/27 bila kugusia mustakabali wa kiungo huyo.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wachambuzi wa soka wanaamini kuwa uzinduzi wa jezi mpya za Yanga unaotarajiwa kufanyika kesho unaweza kuambatana na tangazo kubwa litakalohusisha tetesi hizo. Hata hivyo, hayo yanasalia kuwa maoni ya wachambuzi, kwani hakuna uthibitisho wowote kutoka kwa klabu husika.
