×

Rais Samia Aeleza Umuhimu wa Nishati Safi katika Ukuaji wa Uchumi (Picha +Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, tarehe 05 Agosti, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema upatikanaji wa nishati safi na ya uhakika ni nguzo muhimu katika kukuza viwanda, kupanua biashara na kujenga uchumi wenye ushindani.

Akizungumza Agosti 5, 2026, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Afrika50 na Jukwaa la Miundombinu kwa Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa JNICC jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema maendeleo ya uchumi hayawezi kupatikana bila uwekezaji wa kutosha katika sekta ya nishati.

“Bila upatikanaji wezeshi wa nishati, viwanda haviwezi kukua, biashara haziwezi kutanuka na uchumi hauwezi kushindana,” alisema Rais Samia.

Rais Samia akiwa na viongozi mbalimbali kwenye Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, tarehe 05 Agosti, 2026.

Alieleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika miradi ya nishati safi na salama, ikiwemo uzalishaji wa umeme kupitia maji na gesi asilia, ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika unaochochea ukuaji wa sekta mbalimbali za uzalishaji.

Rais Samia alitaja uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere pamoja na miradi mingine ya vyanzo vya nishati safi kuwa sehemu ya mkakati wa Tanzania wa kuimarisha usalama wa nishati, kulinda mazingira na kuharakisha maendeleo ya viwanda.

Alisisitiza kuwa miundombinu imara ya nishati ni msingi wa kuvutia uwekezaji, kuongeza ushindani wa biashara na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini na barani Afrika kwa ujumla.

 Matukio mbalimbali kwenye kwenye Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, tarehe 05 Agosti, 2026.

Leave a Comment