×

Mshtuko Mexico! TikToker César Gastélum Apigwa Risasi Akiwa Mubashara

Mshawishi maarufu wa TikTok kutoka Mexico, César Gastélum.

Mshawishi maarufu wa TikTok kutoka Mexico, César Gastélum, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi alipokuwa akifanya matangazo ya moja kwa moja (livestream) nje ya mgahawa wa chakula cha haraka katika mji wa Culiacán, usiku wa Agosti 4, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Mexico na Reuters, Gastélum aliyekuwa na zaidi ya wafuasi 600,000 kwenye TikTok, alikuwa pamoja na watu wengine wawili majira ya saa 2:00 usiku kwa saa za eneo hilo, wakati wanaume wawili waliokuwa wamepanda pikipiki walipowakaribia.

Video ya matangazo ya moja kwa moja inaonyesha mshambuliaji akifyatua risasi kuelekea kwa Gastélum. Mwanamitandao huyo, aliyefahamika zaidi kwa video zake za vichekesho, alifariki papo hapo kutokana na shambulio hilo.

Mamlaka za jimbo la Sinaloa zimethibitisha kifo chake na kuanzisha uchunguzi. Vikosi vya Jeshi la Mexico, Polisi wa Jimbo pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Jimbo la Sinaloa alifika eneo la tukio na kuzungushia uzio eneo hilo, kuondoa mwili wa marehemu na kukusanya vielelezo vya uchunguzi.

Hadi sasa, mamlaka hazijatangaza sababu ya mauaji hayo wala kuwataja watuhumiwa.

Kifo cha Gastélum kinakuja wakati jimbo la Sinaloa likiendelea kukumbwa na matukio ya uhalifu na vurugu zinazohusishwa na makundi ya uhalifu uliopangwa. Takwimu zinaonyesha kiwango cha mauaji katika jimbo hilo kiliongezeka kwa karibu asilimia 75 kati ya mwaka 2024 na 2025.

Leave a Comment